1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya ngono Cologne: Serikali ya Merkel mtegoni

6 Januari 2016

Mashambulizi ya kingono ya mkesha wa mwaka mpya nchini Ujerumani yamekoleza mjadala kuhusu uwezo wa nchi hiyo kuwajumuisha idadi kubwa ya wahamiaji, baada ya polisi kuhusisha tukio hilo na watu wenye asili ya Kiarabu.

https://p.dw.com/p/1HZ54
Wakaazi wakindamana mjini Cologne kupinga mashambulizi ya kingono dhidi ya wanawake siku mkesha wa mwaka mpya.
Wakaazi wakindamana mjini Cologne kupinga mashambulizi ya kingono dhidi ya wanawake siku mkesha wa mwaka mpya.Picha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Viongozi wa kisiasa akiwemo Kansela Angela Merkel wamelaani mashambulizi hayo, lakini wameonya pia dhidi ya kutoa hukumu za haraka kuhusu kina nani walihusika. Hata hivyo, kwa baadhi ya Wajerumani ambao hawafurahishwi na wahamiaji milioni moja waliochukuliwa na nchi yao mwaka uliyopita, tukio hilo lilionekana kuthibitisha hofu zao.

Kiongozi wa chama cha kinachopinga wahamiaji cha Alternative für Deutschland, AfD Frauke Petry, alihoji iwapo hii ndiyo Ujerumani aliyoitaka Merkel. Chama chake kimetaka kupunguzwa kwa idadi ya watafuta hifadhi wanaoruhusiwa kuingia nchini, hisia ambazo zinazidi kuongezeka pia miongoni mwa wafuasi wa vyama vya muungano wa Merkel vya mrengo wa kulia.

Meya wa Cologne Henriette Reker na mkuu wa polisi wa mji huo Wolfgang Albers wakiwa kwenye mkutano wa waandishi habari.
Meya wa Cologne Henriette Reker na mkuu wa polisi wa mji huo Wolfgang Albers wakiwa kwenye mkutano wa waandishi habari.Picha: Reuters/W. Rattay

Hofu ya kuchochewa hisia za chuki

Wengine hata hivyo wametahadharisha dhidi ya kulihusisha suala la wakimbizi na uhalifu wa mitaani wakati ukweli wote kuhusu tukio hilo haujulikani.

Waziri wa sheria wa Ujerumani Heiko Maas, alisema kilichotokea usiku huo wa mkesha wa mwaka mpya hakikubaliki hata kidogo, na kwamba wahusika laazima wasakwe na kuwajibishwa, lakini akaongeza kuwa suala hili halihusiani na wapi mtu anatoka, bali alichokifanya.

"Kulihusisha kirahisi suala hili na wakimbizi ni matumizi mabaya ya majdala. Kilicho muhimu kwa sasa ni kubaini ukweli, na kutoa majibu yanayohitajika," alisema waziri Maas.

Meya wa Cologne Henriette Reker, naye aliwambia waandishi wa habari kuwa siyo sahihi kulihusisha kundi la wanaume wanaoonekana kutokea Afrika Kaskazini na wakimbizi, na kufafanua kuwa hakuna ishara zozote kwamba watu waliopatiwa hifadhi Cologne walihusika katika tukio hilo . Nchi zilizoongoza kwa kuwa na waomba hifadhi nchini Ujerumani mwaka uliyopita ni Syria, Albania na Kosovo.

Hakuna aliekamatwa mpaka sasa

Mkuu wa polisi ya mji wa Cologne, Wolfgang Albers, alisema hakuna yoyote aliekamatwa hadi wakati huu, na hivyo hawajui wahusika ni kina nani. Lakini akaongeza kuwa wanachokijua mapaka wakati huu ni kwamba askari polisi waliokuwepo katika eneo la tukio, walihisi wengi wao wao walikuwa vijana wa umri kati ya miaka 18 na 35 kutoka Arabuni au kanda ya Afrika Magharibi.

"Tuliwauliza waathirika iwapo wanaweza kutambua watu na karibu wote walisema hapana, na hii haiturahisishii kazi. Kwa hivyo tunachofanya ni kuchambua picha za video," alisema Albers katika mkutano na waandishi habari na kuitaka jamii itoe ushirikiano kufanikisha kukamatwa kwa wahusika.

Waziri wa Mambo ya ndani wa serikali kuu ya Ujerumani Thomas die Maiziere.
Waziri wa Mambo ya ndani wa serikali kuu ya Ujerumani Thomas die Maiziere.Picha: Imago

Waziri de Maiziere aishukia polisi

Waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu ya Ujerumani Thomas die Maiziere ameilamu polisi mjini humo kwa kushindwa kuzuwia mashambulizi hayo na kutaka apatiwe maelezo ya kina haraka. Awali polisi ilitoa taarifa kuwa sherehe za kuukaribisha mwaka mpya zilipita kwa amani na kwamba hakukuwa na tukio lolote kubwa.

Taarifa za ukubwa wa mashambulizi hayo -- ambayo waathirika walisema yalihusisha vitendo vya kuwatomasa na dai moja la ubakaji -- hakiwekwa hadharani hadi jana Jumanne, wakati malalamiko ya waathirika wa kike yakikaribia kufika 100. Maandamano pia yamefanyika hapo jana mjini Cologne kupinga udhalilishaji huo wa kingono.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre,ape.

Mhariri: Bruce Amani