1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Urusi yawaacha wengi bila umeme, Ukraine

28 Novemba 2024

Zaidi ya Waukraine milioni moja wameachwa bila umeme leo katika mazingira ya baridi kali baada ya Urusi kufanya shambulizi kali la nchi nzima la kombora na droni.

https://p.dw.com/p/4nWES
Ukraine
Mashambulizi ya Urusi yawaacha Waukraine milioni moja bila umemePicha: Jose Colon/AA/picture alliance

Afisa Mkuu mtendaji wa kampuni ya nishati ya Yasno nchini Ukraine, Sergey Kovalenko amesema kuna hali ya dharura ya kukatika umeme kote nchini kutokana na shambulizi la adui kwenye sekta ya nishati.

Shambulizi hilo la pamoja la kombora na droni, lililofanywa kwa awamu saa za alfajiri, lilikata umeme na kuathiri zaidi ya wateja milioni moja magharibi mwa Ukraine.

Viongozi wa NATO wajadili kuimarisha utengenezaji silaha Ukraine

Kiongozi wa mkoa wa Lviv, Maksym Kozytskyi amesema mpaka sasa, watu 523,000 hawana umeme. Mkoa wa magharibi, unaopakana na Poland ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya na NATO, umeepushwa na mapigano makali ya uvamizi wa Urusi wa karibu miaka mitatu.

Hata hivyo umelengwa katika mashambulizi ya mara kwa mara ya makombora na droni ya Urusi. Watu wengine 280,000 wameachwa bila umeme katika mkoa wa magharibi wa Rivne, na wengine 215,000 eneo la kaskazini magharibi la Volyn, linalopakana pia na Poland.