1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi yaendelea Ghouta Mashariki

1 Machi 2018

Serikali ya Syria imeanzisha mashambulizi ya ardhini katika eneo linalodhibitiwa na waasi Ghouta Mashariki, ili kulidhibiti eneo hilo, licha ya mpango wa Urusi wa kusitisha mapigano kwa muda wa saa tano kila siku.

https://p.dw.com/p/2tVCd
Syrien Blutvergießen in Syrien geht weiter - Hilfsorganisationen können Ost-Ghuta nicht erreichen
Picha: Reuters/B. Khabieh

Shirika linalofuatilia haki za binaadamu lenye makao yake nchini Uingereza limesema mashambulizi ya mabomu yamefanyika jana mchana Ghouta Mashariki, huku kukiwa hakuna dalili ya kupelekwa misaada katika eneo hilo ambalo limezingirwa. Hata hivyo shirika hilo limesema hakuna mashambulizi ya anga yaliyofanyika wakati wa kipindi cha muda wa saa tano wa kusitisha mapigano.

Shambulizi la jana lililenga eneo la Hawsh al-Dawahra lililoko ukingoni mwa Ghouta Mashariki. Shirika la haki za binaadamu limeripoti kuwa vikosi vya serikali vinasonga mbele katika eneo hilo na kwamba waasi wengi wameuawa.

Urusi imesisitiza mpango wa kusitisha mapigano kwa muda wa saa tano kila siku ili kuwezesha misaada ya kibinaadamu kupelekwa katika eneo hilo na kuruhusu raia na majeruhi kuondolewa. Hata hivyo, mpango huo wa Urusi ulioanza kutumika siku ya Jumanne ulivunjika saa chache, baada ya kuanza tena kwa mashambulizi ya anga na makombora.

Balozi wa Urusi Vassily Nebenzia
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily NebenziaPicha: picture-alliance/AP/M. Altaffer

Ama kwa upande mwingine, Marekani na Urusi zinatupiana lawama kwa kushindwa kuheshimu mkataba wa kusitisha mapigano Ghouta Mashariki, kwa siku 30 ambao ulipitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumamosi iliyopita.

Balozi wa Marekani anayeshughulikia masuala ya kiuchumi na kijamii katika Umoja wa Mataifa, Kelley Currie ameliambia Baraza la Usalama la umoja huo kwamba Urusi, Iran na utawala wa Rais wa Syria Bashar al-Assad, hawaoneshi jitihada zozote za kuwasihi raia waondoke kwenye eneo hilo, kwa sababu wanataka kushambulia raia waliobaki kwenye eneo hilo la mwisho linalodhibitiwa na waasi.

Urusi inauheshimu mkataba

Akiutetea mpango wa kusitisha mapigano kwa saa tano, balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia amesema nchi yake inafanya kila iwezalo kutekeleza mkataba huo.

''Tunapaswa kufahamu kwamba pande zote zinazohusika zinatakiwa kuutekeleza mpango huu. Lakini inabidi tuelewe bado tutaendelea kuwalenga magaidi katika mashambulizi yetu ya kijeshi,'' alisema Nebenzia.

Aidha, jeshi la Urusi limesema leo kuwa raia wa Ghouta Mashariki wametoa maombi kadhaa ya kuondolewa kwenye eneo hilo. Kamanda wa jeshi la Urusi, Meja Jenerali Vladmir Zolotukhin amesema kuwa waasi wanaendelea kushambulia njia inayopaswa kutumika kuwaondoa raia kutoka Ghouta Mashariki.

Juhudi za uokozi zikiendelea
Mwanamke akiokolewa kutoka kwenye kifusi Ghouta MasharikiPicha: picture alliance/abaca/A. Al Bushy

Hayo yanajiri wakati ambapo Urusi ikisema Marekani imeweka kiasi ya kambi 20 za kijeshi kwenye eneo linalodhibitiwa na Wakurdi nchini Syria na kwamba Marekani inawapatia Wakurdi silaha za kisasa.

Wakati huo huo, malori 40 yaliyobeba msaada wa kibinadamu yako tayari kusafirisha shehena hiyo kuingia Ghouta Mashariki. Mkuu wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa, Mark Lowcock, amesema hali katika eneo la Ghouta Mashariki haijabadilika na mashambulizi ya mabomu yanaendelea, licha ya kuwepo azimio la kusitisha mapigano. Lowcock amesema misaada haijapelekwa kwenye eneo hilo, wala raia hawajaondolewa na kwamba idadi ya vifo inaongezeka.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA, Reuters, DW http://bit.ly/2FgTGRD
Mhariri: Saumu Yusuf