1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi yaendelea Syria licha ya azimio la UN

25 Februari 2018

Serikali ya Syria imefanya mashambulizi makubwa ya anga na ardhini katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi Ghouta Mashariki, siku moja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kusitishwa haraka mapigano.

https://p.dw.com/p/2tJHL
Syrien Damaskus - Ost-Ghuta: Verwüstung nach Luftangriffen
Picha: picture-alliance/AA/Q. Noor

Shirika linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake Uingereza, limesema kuwa kiasi ya watu 13 wanaoviunga mkono vikosi vya serikali na wapiganaji sita wa kundi la waasi wa Jaish al-Islam, wameuawa katika mashambulizi yaliyofanywa leo.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Rami Abdel Rahman amesema mapigano yanafanyika katika eneo la Al-Marj ambalo ni eneo la mapambano linalodhibitiwa na waasi karibu na mji mkuu wa Syria, Damascus.

Zaidi ya raia 500 wauawa tangu kuanza mapigano

Ameongeza kusema kuwa mashambulizi ya leo ni mabaya zaidi kufanyika tangu utawala wa Syria ulipoanzisha operesheni mwezi huu wa Februari. Zaidi ya raia 500 wameuawa katika operesheni hiyo iliyoanzishwa wiki iliyopita Mashariki mwa Ghouta.

Mashambulizi hayo yanafanyika siku moja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupiga kura kwa kauli moja kutaka kusitishwa mapigano nchini Syria kwa siku 30 na kuruhusu kupelekwa misaada ya kibinaadamu na kuwaondoa raia kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

UN Sicherheitsrat Abstimmung über Waffenruhe in Syrien
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakipiga kuraPicha: picture alliance/ZUMAPRESS.com

Hayo yanajiri wakati ambapo Urusi imesema kuwa inavitegemea vikosi vya kigeni vinavyoipinga serikali ya Syria kuhakikisha mapigano yanasitishwa kama ilivyopendekezwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana. Taarifa iliyoandikwa katika tovuti ya wizara ya mambo ya Urusi imeeleza kuwa nchi hiyo imeyataka makundi hayo kusitisha mapigano ili kuruhusu kupelekwa misaada ya kibinaadamu.

Kwa upande wake kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ametoa wito wa kusitishwa haraka mapigano nchini Syria na kuruhusu kupelekwa misaada ya kiutu, hasa kwenye eneo linalodhibitiwa na waasi, Ghouta Mashariki ambalo limekuwa likishambuliwa na vikosi vya serikali.

Akizungumza leo wakati akiwabariki waumini, Papa Francis amesema katika miaka saba ya machafuko nchini Syria, mwezi huu wa Februari umekuwa wenye machafuko zaidi na huo ni ukatili. Ameongeza kusema kwa mtu hawezi kupambana na uovu kwa kutumia uovu mwingine.

Hata hivyo, Iran imesema itaendelea na mashambulizi katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi karibu na Damascus, kwa sababu azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutaka kusitishwa vita Ghouta Mashariki halikuyalenga makundi ya kigaidi.

Iran inaliheshimu azimio

Shirika la habari la Iran, IRNA limetangaza kuwa Iran imesema inaliheshimu azimio la kimataifa na serikali ya Syria pia inaliheshimu, lakini maeneo yanayodhibitiwa na Al-Nusra na makundi mengine ya kigaidi hayajalengwa na azimio hilo la kusitisha mapigano, hivyo operesheni za jeshi la Syria, zitaendelea kwenye maeneo hayo.

Aidha, Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki, Bekir Bozdag amesema kuwa azimio lililopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kusitisha mapigano halitoathiri operesheni inayofanywa na Uturuki dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi katika mkoa wa Afrin.

G20-Gipfel Gespräch  Merkel Putin Macron
Rais Macron, Rais Putin na Kansela MerkelPicha: picture alliance/dpa/T. Schwarz

Wakati huo huo, viongozi wa Urusi, Ufaransa na Ujerumani wamekubaliana kuharakisha hatua ya kubadilishana taarifa kuhusu Syria. Taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel imeeleza kuwa makubaliano hayo yamefikiwa katika mazungumzo kwa njia ya simu kati ya Rais wa Urusi, Vladmir Putin, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron pamoja na Kansela Merkel.

Viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi za pamoja katika kutekelezwa haraka iwezekanavyo azimio la Umoja wa Mataifa la kusitisha mapigano Ghouta Mashariki. Merkel na Macron wamesisitiza kuwa kusitishwa mapigano kunaweza kuwa msingi wa kuendeleza juhudi za kupatikana suluhisho la kisiasa katika mchakato wa amani ya Syria unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

''Ujerumani na Ufaransa ziko tayari kuendelea kushirikiana na Urusi na washirika wengine wa kimataifa ili kulifanikisha lengo hilo,'' ilifafanua ofisi ya Merkel.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, Reuters
Mhariri: John Juma