Mashambulizi yatokea tena karibu na kinu cha Zaporizhzhia
28 Agosti 2022Taarifa hizo za mashambulizi ya usiku wa kuamkia leo zimetolewa na maafisa wa serikali za maeneo ya miji na ripoti hizo zimezidisha mashaka miongoni mwa wakazi wa maeneo jirani na kinu cha Zaporizhzhia.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema siku ya Jumapili kwamba ni Ukraine ndiyo inarusha makombora kukilenga kinu hicho.
Kulingana na wizara hiyo, makombora kadhaa ya Ukraine yamekilenga kituo hicho cha kuzalisha umeme ndani muda wa saa 24 zilizopita.
Mwenendo huo wa kulaumiana kati ya Moscow na serikali mjini Kyiv juu ya upande unaohusika na mashambulizi karibu na kinu cha Zaporizhzhia unazidisha hamkani kwa Jumuiya ya Kimataifa.
Usalama wa kinu hicho cha nyuklia ambacho ndiyo kikubwa zaidi barani Ulaya, ni jambo linaloyashughulisha mataifa mengi duniani hivi sasa.
Wakaazi wapewa mbinu za kujikinga na mionzi ya nyuklia
Kampuni ya nishati ya nyuklia ya Ukraine, Energoatom, imesema haina taarifa zozote mpya kuhusu mashambulizi kwenye kinu cha Zaporizhzhia.
Kituo hicho kilichokamatwa na vikosi vya Urusi mnamo mwezi Machi bado kinaendeshwa na wafanyakazi wa Ukraine.
Hata hivyo mapigano karibu na eneo hilo yamekifanya kuwa moja ya maeneo yanayotizamwa kwa jicho la karibu katika mzozo wa miezi sita tangu Urusi ilipotuma jeshi lake nchini Ukraine.
Gavana wa jimbo la Zaporizhzhia Oleksandr Starukh amearifu kupitia mtandao wa Telegram kwamba vikosi vya Urusi vimeyalenga makaazi ya watu kwenye mji mkubwa zaidi wa jimbo hilo uliopo umbali wa masaa mawili kwa usafiri wa gari kutoka kinu cha Zaporizhzhia. Mji mwingine mdogo wa mashariki wa Orikhiv pia umeshambuliwa.
Mnamo siku ya Jumamosi, Starukh alikiambia kituo kimoja cha televisheni nchini Ukraine kwamba wakaazi karibu na kinu hicho wamekwishapewa maelekezo ya kutumia kiambata cha kemikali ya iodine kutakachopunguza madhara iwapo kutatokea mkasa wa kuvuja kwa mionzi ya nyuklia.
Umoja wa Mataifa wataka pande zote ziondoe vikosi karibu na kinu hicho
Jeshi la Ukraine limeripoti juu ya kushambuliwa kwa miji mingine tisa katika eneo mkabala na mto Dnipro uliopo karibu na kinu cha Zaporizhzhia.
Shirika la habari la Urusi RIA limeinukuu wizara ya ulinzi ya nchi hiyo ikisema jeshi lake la anga lilikishambulia kituo cha kuunda mota za umeme eneo ambako helikopta zilikuwa zikitengezwa.
Taarifa zote hizo hazikuweza kuthibitishwa na shirika la habari la Reuters kutokana na ugumu wa kuyafikia maeneo hayo.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi Igor Konashenkov amesema makombora tisa yalifyetuliwa na jeshi la Ukraine katika mkasa wa mashambulizi mawili tofauti.
Kulingana na afisa huyo makombora hayo yalianguka kwenye eneo la kinu cha Zaporizhzhia. Umoja wa Mataifa umerejea wito wake wa kuzitaka pande kuondoa vikosi vyao kutoka kinu hicho.