Mashirika ya ndege yaungana Somalia
19 Februari 2015Shirika la Daallo Airlines na Jubba Airways kwa miaka mingi yamekuwa yakipata faida peke yao bila ushindani katika mojawapo ya soko lenye changamoto kubwa duniani, yakishindana katika njia za angani kuelekea Somalia, taifa ambalo mashirika mengi yamekuwa yakilikwepa kutokana na vita.
Huku vita vikiendelea kutulia nchini Somalia mashirika ya ndege ya kanda hiyo Daallo Airlines na Jubba Airways yanakabiliwa na mashindano mapya ambayo yameyalazimu kuungana - ushindani kutoka kwa mashirika makubwa ya kimataifa kama vile Shirika la ndege la Uturuki, Turkish Airlines, Shirika la ndege la Ethiopia, Ethiopian Airlines, na flydubai, yanayoendesha safari zao katika anga ya Somalia.
Mashirika ya Daallo na Jubba ambayo hutoa huduma za safari za ndani nchini Somalia, lakini yanayokabiliwa na changamoto nyingi katika safari za kimataifa, leo yanatarajiwa kuzindua muungano kwa jina African Airways Alliance, utakaomikiliwa sawasawa na waanzilishi wa mashirika yote mawili.
"Mambo yanatuendea kinyume, lakini hiyo ndio sababu kwa nini tunaungana, amesema Mohamed Yassin, Mkurugenzi mkuu wa shirika la ndege la Daallo, wakati alipozungumza na shirika la habari la Reuters. Yassin aidha amesema "Hatukai tu kitako. Tunajaribu kuunganisha nguvu zetu pamoja kukabiliana na changamoto mpya zilizojitokeza."
Katika mahojiano aliyoyafanya mjini Nairobi Kenya akiwa pamoja na mwenyekiti wa shirika la ndege la Jubba, Said Qailie, Yassin pia alisema, "Tunajaribu kuyavutia mashirika mengine ya ndege kujiunga na muungano huo kuimarisha biashara, kusaidia ukuaji na uthabiti." Aliongeza kusema kuwa mashirika yote mawili yataendelea kutumia nembo zao baada ya muungano huo kuzinduliwa.
Mipango ya baadaye
Kwa pamoja mashirika ya Daallo na Jubba yamesema katika taarifa kwamba yaliwabeba abiria 250,000 mwaka uliopita na kukusanya mapato ya zaidi dola milioni 75 za kimarekani. Kwa kulinganisha shirika la ndege la Uturuki, Turkish Airlines, liliwabeba abiria milioni 54.7 mwaka jana.
Shirika la Daallo linamilikiwa kibinafsi na shirika la ndege la kitaifa la Djibouti, kaskazini mwa Somalia, huku shirika la Jubba likiwa limesajiliwa nchini Kenya upande wa kusini. Hakuna shirika rasmi la ndege la Somalia baada ya shirika la ndege la nchi hiyo, Somali Airlines, kusitisha huduma zake mnamo mwaka 1991 wakati vita vilipopamba moto nchini humo. Yassin ameieleza Somalia kuwa soko la nyumbani kwa mashirika hayo mawili baada ya kutimiza jukumu kubwa muhimu na kutoa msaada wakati wa vita.
Baada ya muungano kuzinduliwa mashirika hayo yataendesha safari kutumia ndege mpya zilizokodiwa aina ya Airbus A321-111s na Boeing 737-300. Pamoja na hayo kampuni hiyo itatumia ndege aina ya BAe 146-200, inayoimiliki, kwa huduma za safari binafsi. Kufikia katikati ya mwaka huu, ndege mbili aina ya turboprop ATR zitazinduliwa kwa ajili ya safari za ndani ya Somalia.
Mwaka huu pia muungano huo mpya unapania kuongeza idadi ya vituo vya safari kutoka 13 hadi 21. Vituo vya safari vilivyopo kwa sasa ni pamoja na Nairobi, Kenya, Dubai na Jeddah, Saudi Arabia. Vituo vinavyopangwa ni Addis Ababa, Ethiopia , viwanja vya ndege nchini Yemen, Kampala, Uganda na miji mikubwa ya Ulaya.
Changamoto ya mashirika mengine
Wajasiriamali wanaomiliki mashirika ya ndege, makampuni ya kutuma fedha na kampuni za simu za mkononi walifanya uvumbuzi na kunawiri nchini Somalia kwa zaidi ya miongo miwili, na kuwaweka Wasomali katika mawasiliano na ulimwengu wakati taifa hilo liliposambaratishwa na wababe wa kivita na wanamgambo wa kiislamu.
Sasa serikali ya shirikisho ya Somalia mjini Mogadishu inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa polepole inatanua udhibiti wake na kurejesha utangamano na uthabiti wa kisiasa, ambao pia unayabadili mazingira ya kibiashara ya kampuni kama Daallo na Jubba ambazo awali zilikuwa zikinufaika peke yao kutokana na soko la Somalia.
Shirika la ndege la Uturuki, Turkish Airlines, sasa linatoa huduma ya kila siku kwenda Mogadishu, huku shirika la ndege la Ethiopia, Ethiopian Arlines, likiendesha safari kwenda Hargeisa katika eneo la kaskazini lenye utawala wake wa ndani la Somaliland, kituo ambacho shirika la ndege la flydubai linapanga kuanzisha safari zake kuanzia mwezi ujao. Shirika la ndege kutoka Kenya, African Express, pia linafanya safari kwenda Mogadishu na miji mingine ya Somalia.
Shirika la ndege la Uturuki, Turkish Airlines, lilitangaza mwezi uliopita kwamba lilikuwa limeongeza safari zake kwenda Mogadishu kutoka nne hadi saba kwa wiki, lakini likasema halina mipango ya haraka ya siku za usoni kuongeza vituo vingine vya safari zake nchini Somalia.
Mwandishi: Josephat Charo/RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman