Masikini washambulia masikini wenzao Afrika Kusini
23 Mei 2008Maeneo wanakoishi watu masikini yamekuwa kama eneo la vita.Wahamiaji walianza kufukuzwa kutoka vitongoji vya jiji la Johanesburg na sasa machafuko hayo yameenea katika miji mingine.Mashambulizi hayo ya chuki yanawalenga wakimbizi kutoka Zimbabwe,Msumbiji,Malawi na wahamiaji wengine wanaoishi bila ya vibali.Wakimbizi hao wanalaumiwa na wazalendo kusababisha umasikini, ukosefu wa ajira na nafasi za kujielimisha na kujiendeleza.Hayo ni maoni ya magenge ya wahuni wanaowashambulia wageni nchini Afrika Kusini.
Machafuko yaliyoibuka Afrika Kusini ni matokeo ya kutofanikiwa kwa sera za kisiasa.Sifa kuwa Afrika Kusini ni taifa lenye mchanganyiko wa mataifa mbali mbali hailingani kabisa na ukweli wa kisiasa na kijami.Kila Mwaafrika Kusini wa tatu hana ajira-wanaonufaika na ukuaji wa kiuchumi nchini humo hasa ni watu wa tabaka ya juu,huku nusu ya wazalendo wakijikuta katika hali ya umasikini zaidi kuliko hiyo miaka 14 iliyopita.Sasa vile vile kuna tatizo jipya la kuongezeka kwa bei za vyakula na mafuta.Katika hamaki yao,masikini wamewashambulia masikini wenzao.
Wimbi hilo la mashambulizi likiendelea,serikali ndio imeamua kutumia majeshi kudhibiti machafuko na kurejesha utulivu nchini.Lakini ili kujiepusha na utulivu wa juu juu tu,viongozi wa Afrika Kusini wanapaswa kuchangamka na kuchukua hatua kuhusu sera zake za ndani na nje.Kwani wimbi la wakimbizi kutoka Zimbabwe limesababishwa na janga la kiuchumi linalokutikana katika nchi hiyo.Lakini Afrika Kusini inaendelea na kile kinachoitwa udiplomasia wa pole pole kuhusika na Rais Robert Mugabe.Afrika Kusini iache kubeba mzigo wa Zimbabwe na kumuunga mkono Mugabe kiuchumi na kisiasa.Kwani kwa sehemu fulani mzozo wa wakimbizi unahusika na sera za nje za kutoingilia kati.
Afrika Kusini katika sera zake za nje isibakie kimya na kutazama jinsi serikali ya Mugabe inavyowakamata na kuwatesa wapinzani wake na kuwafanya wananchi wahanga wa sera zake.Wanasiasa wa Afrika Kusini wanapaswa kuchangamka ili Mashindano ya Ubingwa wa Kandanda Duniani mwaka 2010 yatakapowadia,nchi hiyo itakuwa yenye usalama,furaha na watu wa aina mbali mbali.