Masoud Pezeshkian ashinda uchaguzi wa rais Iran
6 Julai 2024
Mgombea wa urais mwenye msimamo wa wastani wa kisiasa nchini Iran, Masoud Pezeshkian ameshinda uchaguzi wa raisi katika duru ya pili dhidi ya mhafidhina Saeed Jalili.
Matokeo hayo yaliyotangazwa na Wizara ya mambo ya ndani yanaonyesha kuwa Pezeshkian alipata zaidi ya kura milioni 16 na Jalili zaidi ya milioni 13 kati ya kura milioni 30 zilizopigwa. Msemaji wa mamlaka ya uchaguzi Mohsen Eslami alisema watu waliojitokeza kupiga kura ilifikia asimilia 49.8.
Soma zaidi. Iran wapigakura duru ya pili kumchaguwa rais.
Viongozi mbalimbali duniani akiwemo rais Vladmir Putin wa Urusi na uongozi wa Saudi Arabia wametuma salamu za pongezi kwa mwanamageuzi huyo kwa kuchaguliwa kuwa rais wa Iran.
Masoud Pezeshkian ameutumia mtandao wa X kuwashukuru watu wa Iran kwa kumchagua. Itakumbukuwa kuwa uchaguzi huo, uliitishwa baada ya kifo cha rais wa Iran Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta.