Maswali yaibuka kuhusu miili 11 ilopatikana Mto Tana Kenya
13 Septemba 2021Kwa muda wa miezi mitatu sasa maiti kumi na moja zimeopolewa kutoka mto huo huku baadhi yake zikiwa zimefungiwa kwenye mawe makubwa. Idara ya polisi inasema inafanya uchunguzi wa vinasaba kuweza kuwatambua watu hao ila jambo hilo linakuwa gumu kutokana na miili hiyo kuoza.
Seneta wa jimbo la Mombasa Mohammed Faki amezikosoa idara za usalama kwa kuwa kimya juu ya jambo hilo ambalo limekuwa kama desturi kwa watu kupotea na baadaye kupatikana wameuliwa kinyama. Kiongozi huyo amesema atapeleka mswada bungeni wa kutaka wizara ya usalama kushurutishwa kuwajibika.
Mjini Mombasa na Lamu familia zimekuwa zikitoa taarifa za watu wao kutekwa nyara, familia hizo kwa sasa zimeombwa kufika katika idara ya usalama na hospitali ya Garisa ili wafanyiwe ukaguzi wa kimaabara ndio ulinganishwe na vinasaba vya maiti hao.
Naibu kiongozi wa baraza kuu la waisilamu nchini Kenya Sheikh Moudhar Khitamy ameitaka serikali kuwajibika katika kadhia hii inayoendelea huku akidai wanaolengwa ni jamii ya Waisilamu.
Mkuu wa idara ya upelelezi nchini Kenya George Kinoti ametoa taarifa akisema kuwa wameanzisha uchunguzi.
Mwandishi: Faiz Musa/DW/Mombasa
Mhariri: Iddi Ssessanga