1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa makubwa kinyuklia yaahidi kuzuia silaha za nyuklia

4 Januari 2022

Mataifa matano yenye nguvu kubwa kinyuklia ulimwenguni yameahidi kuzuia ongezeko zaidi la silaha za nyuklia na kusema vita vya nyuklia haviwezi kuwa chaguo na ni lazima vizuiwe kwa nguvu zote.

https://p.dw.com/p/456Sc
Russland | Videostill von RU-RTR - Neue Interkontinentalrakete
Picha: AP Photo/picture-alliance

Mataifa hayo yamesema silaha za nyuklia zinatakiwa kutumika kwa ajili ya ulinzi, kuzuia uingiliaji na hata vita. 

Ahadi hiyo imetolewa kabla ya mapitio ya kumi na ambayo ni ya karibuni zaidi ya mkataba wa kuzuia kuongezeka kwa silaha za nyuklia ama NPT yaliyopangwa kufanyika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mwezi huu, lakini yaliahirishwa hadi baadae mwaka huu.

Taarifa ya pamoja na ya nadra ya mataifa hayo matano yenye nguvu kubwa kinyuklia ulimwenguni ambayo ni China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani imetolewa jana Jumatatu. Kwa pamoja yameahidi kuzuia kuongezeka kwa silaha hizo za nyuklia na kuongeza kuwa wana imani thabiti kwamba kuna umuhimu mkubwa wa kuzuia kusambaa zaidi kwa silaha kama hizo.

Soma Zaidi: Ufaransa yatilia mashaka mazungumzo ya nyuklia ya Iran

Kwenye taarifa hiyo, mataifa hayo yamesema badala yake silaha za nyuklia zinatakiwa kutumika kwa shughuli za ulinzi, kuzuia uingiliaji pamoja na vita.

Mataifa hayo matano ambayo ni wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa yamekubaliana pia kufanya mazungumzo kwa nia njema kuhusiana na hatua madhubuti za kusitisha ushindani wa kuzitengeneza, pamoja na kuzipokonya silaha hizo, lakini pia mkataba wa utekelezwaji wa hatua hizo chini ya udhibiti mkali wa kimataifa.

UN Vollversammlung NO FLASH
Mataifa hayo matano pia ni wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/dpa

China na Urusi zasifu hatua hiyo.

Shirika la habari la China, Xinhau limemnukuu waziri wa mambo ya kigeni wa China Ma Zhauxu akisema makubaliano hayo yatasaidia kuongeza hali ya kuaminiana na kuziba ombwe linaloletwa na ushindani miongoni mwa mataifa hayo, kwa kushirikiana na kuyaratibu kwa pamoja.

Urusi nayo imesema kupitia wizara yake ya mambo ya kigeni kwamba wanatarajia kuidhinishwa kwa taarifa kama hiyo ya kisiasa kutasaidia kupunguza kiwango cha wasiwasi ulimwenguni, katika mazingira magumu kama ya sasa yahusuyo usalama wa kimataifa.

Mkataba wa NPT ni wa kimataifa ulioundwa kwa lengo la kuzuia kusambaa kwa silaha za nyuklia na zilizoundwa kwa teknolojia ya kisasa, wakati mataifa yakisaka namna ya kufikia hatua ya kuzuia kabisa usambaaji huo. Ulianza kutumika mwaka 1970 baada ya mataifa wanachama 191 kutiliana saini mwaka 1968.

Afrika Kusini ni taifa pekee lililotengeneza silaha hizo na baadae kuziharibu kabisa, wakati Korea Kaskazini ikiwa imejitoa kwenye mkataba huo.

Hata hivyo taarifa hii inatolewa katikati ya mivutano mikali baina ya mataifa hayo makubwa, ambayo ni pamoja na kati ya Marekani na Urusi, kutokana na Urusi ya kujiimarisha kijeshi katika mpaka wa Ukraine hadi Marekani na China wanaozozana kuhusu hadhi ya Taiwan na kuongezeka kwa shughuli za kijeshi katika eneo la Pasifiki.

Mashirika: DW