1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa makuu yataka kusitisha mapigano Libya

17 Julai 2019

Mataifa makubwa yakiwemo yanayomuunga mkono kiongozi wa waasi yametoa wito wa kusitishwa mapigano nchini Libya, yalionya kuwa umuagaji damu unazidisha hali ya kibinadamu ambayo imeelezwa kuwa janga tayari.

https://p.dw.com/p/3MBia
Libyen Bürgerkrieg
Picha: picture-alliance/dpa/EPA/M. Messara

Marekani, Ufaransa, Uingereza na Italia zimeungana na Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu - mataifa mawili ambayo kwa pamoja na Saudi Arabia yanamuunga mkono mbabe wa kivita Khalifsa Haftar - katika kuelezea wasiwasi juu ya machafuko yanayoendelea katika mji mkuu wa Libya Tripoli.

Mataifa hayo sita "yanatoa wito wa kupunguza mara moja mzozo na kusitisha mapigano ya sasa, na yanahimiza kurejea kwenye mchakato wa kisiasa unaoongozwa na Umoja wa Mataifa," ilisema taarifa ya pamoja.

Wameonya kuwa mapigano yamechochea dharura inayoongezeka ya kibinadamu, kuzidisha mzozo na wahamiaji, na kuelezea hofu kwamba makundi ya itikadi kali yatashamiri kukiwa na ombwe la usalama.

Nchi moja, serikali mbili

Libya imegawika kati ya serikali ya maridhiano ya kitaifa mjini Tripoli, ambayo inaungwa mkono na Umoja wa Mataifa, na serikali ya mjini Tobruk inayoongozwa na Marshal Khalifa Haftar.

Libyen Tripolis nach dem Luftangriff auf das Tajoura Detention Center
Kituo cha kuwazuwia wahamiaji wa Kiafrika kilishambuliwa katika kampeni ya Haftar kuutwa mji mkuu Tripoli, Julai 3, 2019.Picha: Getty Images/AFP/M. Turkia

Haftar pia anaudhibiti mji wa mashariki ya Benghazi ambako wakaazi wake waliandama Jumapili kupiga madai ya Uturuki kuiunga mkono serikali ya mjini Tripoli. Muftah Mohamed alikuwa mojawapo wa washiriki wa maandamano hayo na anasema:

"Tunaliunga mkono jeshi la LNA, tunatoa wito wa kususiwa Uturuki, Fayez Surraj na majambazi na wahalifu wote mjini Tripoli. Na sisi ni washindi, na kutoka ushindi hadi ushindi, bado tunalipa gharama. Hatumuogopi yeyote, hatuiogopi Uturuki, tumeunda jeshi imara na polisi.

Zaidi ya watu 1,000 wauwa katika mwezi mmoja

Karibu watu 1,100 wameuawa katika kampeni ya Haftar iliyodumu kwa mwezi mmoja akijaribu kuutwa mji mkuu Tripoli kutoka serikali ya maridhiano ya kitaifa inayotambuliwa na Umoja wa Matifa.

Licha ya kuinga mkono serikali mjini Tripoli, mataifa ya magharibi mapema mwaka huu yalituma ishara mchanganyiko, huku rais wa Marekani Donald Trump akimsifu Haftar katika mazugumzo kwa njia ya simu, na Ufaransa na itali zikimkaribisha kwa ziara.

Hapo jana mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Ghassan Salame alikutana na waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan mjini Abdu Dhabi, kujadili njia za kumaliza mapigano nchini Libya.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe

Mhariri: Josephat Charo