Mataifa tajiri kujadili mustakabali wa EU
6 Machi 2017Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na Rais wa Ufaransa, Francois Hollande ambao nchi zao zinatajwa kama injini ya Umoja wa Ulaya, wataungana na Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy na Waziri Mkuu wa Italia, Paolo Gentiloni. Duru za kidiplomasia kutoka Ufaransa zinaeleza kuwa lengo la mkutano huo ni kujaribu kuangalia hali ya kisiasa katika mataifa hayo manne.
Mkutano huo unafanyika siku chache kabla ya kuadhimishwa kwa miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa Roma uliosababisha kuanzishwa kwa Umoja wa Ulaya. Maadhimisho hayo yatafanyika tarehe 25 ya mwezi huu wa Machi. Tarehe hiyo, ukiunganisha na matokeo ya kura ya maoni ya Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, Brexit na kuongezeka kwa siasa za kizalendo, vimechochea kuongezeka kwa wasiwas kuhusu mustakabali wa Ulaya.
Ujerumani na Ufaransa zimesema changamoto kuhusu Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya, ambazo zinakuja baada ya mzozo wa sarafu ya Euro, uhamiaji na mzozo wa Ukraine, unazifanya zitafute nguvu mpya kwa lengo la kuimarisha mamlaka ya Umoja wa Ulaya kwa dharura kuliko wakati mwingine wowote ule.
Ulaya inakabiliwa na uchaguzi wa wabunge nchini Uholanzi baadae mwezi huu na kufuatiwa na uchaguzi wa urais nchini Ufaransa mwezi Aprili na Mei. Ujerumani, nchi yenye uchumi mkubwa barani Ulaya, itafanya uchaguzi wake wa bunge mwezi Septemba.
Mgombea wa urais kupitia chama cha siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ufaransa, Marine Le Pen, anatabiriwa kufika katika duru ya pili ya uchaguzi wa Ufaransa, wakati chama kinachopinga Uislamu cha nchini Uholanzi cha Mbunge Geert Wilders, kikitarajiwa kufanya vizuri katika uchaguzi. Wakati huo huo, Merkel anakabiliwa na shinikizo kutoka kwa chama mbadala kwa Ujerumani AfD kinachopinga wahamiaji ambacho kinafuata siasa kali za mrengo wa kulia.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker, amependekeza katika ''Waraka Maalum'' unaoonyesha mpango wake kuhusu mustakabali wa umoja huo. Katika muktadha huo, nchi ambazo zinataka kuendelea na masuala kama vile ukuaji wa uchumi, kulinda mipaka na ulinzi, zinaweza kuanzisha makundi madogo na kuwaacha nyuma wanachama ambao hawazungumzi mambo mengi.
Italia, Ubelgiji, Uholanzi na Luxembourg zimesaini mpango wa kasi za aina nyingi, kutokana na kuwa na hofu kuhusu kuongezeka kwa vyama vinavyoipinga Ulaya. Lakini katika kuepuka mataifa wanachama ambayo yanaleta upinzani, yakiwemo mengi kutoka Ulaya Mashariki, hakuna mradi madhubuti ambao unatarajiwa kutangazwa baada ya mkutano huu wa leo unaofanyika Ufaransa.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf