Mataifa ya Afrika yatafuta sauti zaidi katika mzozo wa Libya
18 Januari 2020Mataifa ya bara Ulaya, Uturuki na Urusi, yatashiriki katika kongamano la amani la Libya mjini Berlin wikendi hii, hizi zikiwa juhudi za hivi punde za kimataifa za kutamatisha mapigano kati ya kamanda wa eneo la Mashariki Khalifa Haftar na serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa mjini Tripoli.
Mwenyekiti wa Muungano wa Afrika Moussa Faki pia atashiriki katika mazungumzo hayo ya Berlin na kutumaini kuleta mtazamo wa bara Afrika lakini halitakuwa jukumu rahisi. Kulingana na msemaji wa Faki, Ebba Kalondo, mataifa jirani kama Chad, Sudan, Algeria, Tunisia, Misri na zaidi yanaathirika kutokana na athari hizo.
Kulingana na Kalondo, Muungano wa Afrika umekuwa ukiulizia jukumu zaidi katika harakati zinazoendelea lakini mara kwa mara umepuuzwa. Kwa muda mrefu, eneo la Sahel na mataifa ya Afrika yamekuwa yakiathirika kutokana na mzozo wa Libya.
Baada ya upande wa uasi ulioungwa mkono na jumuiya ya kujihami ya NATO kumuondoa mamlakani na kumuuwa dikteta Muammar Gadhafi mnamo mwaka 2011, Libya ilitumbukia katika mzozo wa makundi ya kijeshi kushindania mamlaka. Katika ghasia hizo, wanamgambo wa kiislamu na wasafirishaji wa wahamiaji wakapanua ushawishi wao.
Pengo la usalama nchini Libya liliwezesha kusambaa kwa wapiganaji, silaha na vilipuzi katika mipaka yake na kuingia nchini Mali, Niger na Burkina Faso ambazo zinakabiliwa na ongezeko la ghasia za kijihadi licha ya kampeini ya kanda hiyo kukabiliana na wanamgambo hao wa kiislamu. Taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika bado limesalia katika mizozo ambayo kwasasa ni kati ya vikosi vinavyoongozwa na Haftar katika eneo la Mashariki na serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa ya Tripoli. Vikosi vinavyoongozwa na Haftar vilitekeleza mashambulizi katika mji mkuu wa nchi hiyo mnamo mwezi Aprili.
Mwezi Desemba mwaka uliopita, rais wa Niger Mahamadou Issoufou, alisema kuwa jamii ya kimataifa inahusika katika kile kinachoendelea katika eneo hilo kupitia maamuzi mabaya ya kuingilia Libya, akimaanisha kampeini ya NATO ya mwaka 2011.Ameliambia shirika la AFP kwamba Libya iko Afrika na tatizo la Libya haliwezi kutatuliwa kwa kuutenga Muungano wa Afrika.Rais wa Chad Idriss Deby, amesema kuwa kutatuliwa kwa mzozo wa eneo la Sahel kunahusika moja kwa moja katika kutamatisha hali ya msukosuko nchini Libya.
Mnamo mwaka 2019, kundi la kijihadi liliwauwa watu elfu 4 nchini Burkina Faso, Mali na Niger licha ya kuweko kwa maelfu ya vikosi vya ufaransa , ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali na muungano wa G5 wa Sahel miongoni mwa majeshi ya mataifa matano ya kanda hiyo.
Kulingana na mwanadiplomasia mmoja kutoka Ulaya, ''Afrika inatafuta kusikilizwa zaidi hivi sasa huku hali ya usalama ikiendelea kudorora katika eneo la Sahel.'' Lakini Umoja wa Mataifa unaandaa mazungumzo hayo ya Berlin na kuchukuwa jukumu muhimu katika mazungumzo hayo. Kulingana na Claudia Gazzini wa shirika la mizozo ya kimataifa, hali hii inasalia katika mikono ya Umoja wa Mataifa na chini ya uongozi wa Umoja wa Mataifa na hivyo inamaanisha kuwa Muungano wa Afrika umepuuzwa.