1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Ghuba yako tayari kuzungumza na Qatar

31 Julai 2017

Mataifa manne ya Kiarabu yaliovunja uhusiano na Qatar yamesema yako tayari kwa mazungumzo ya kutatua mzozo huo ikiwa Doha itaonyesha nia ya kushughulikia madai yao. Qatar imesema huo ni upotoshaji wa jamii ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/2hRzw
Bahrain Außenminister von VAE, Saudi Arabien und Ägypten
Picha: picture-alliance/abaca/Stringer

Kundi la mataifa hayo linaloongozwa na Saudi Arabia lilikata mahusiano na Qatar Juni 5, wakiituhumu kwa kuyaunga mkono makundi ya wanamgambo na kushirikiana na hasimu wao mkuu wa kikanda  Iran, madai ambayo serikali mjini Doha inayakanusha vikali.

Juhudi za kidiplomasia za Kuwait na zinazoungwa mkono na mataifa ya magharibi zimeshindwa mpaka sasa kukomesha mzozo huo, ambao unahusisha kuwekewa vikwazo vya usafiri na mawasiliano Qatar  na mataifa hayo manne.

Wasema Qatar haina ni ya kusuluhisha

Saudi Arabi na washirika wake awali walitoa orodha ya  madai 13 kwa Qatar, ambayo yanahusisha kuitaka nchi hiyo kukomesha uungaji wake mkono kwa kundi la Udugu wa Kiislamu, kufunga kituo cha Televishen cha Al Jazeera chenye makao yake mjini Doha, kufunga kambi ya kijeshi ya Uturuki, na kushusha kiwango cha uhusiano na adui wa mataifa ya Ghuba Iran.

Katar Außenminister von Saudi Arabien Adel bin Ahmed Al-Jubeir in Manama
Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Adel bin Ahmed Al-Jubeir akizungumza na waandishi habari mjini Manama Jumapili, 30.07.2017.Picha: Reuters/H. I. Mohammed

Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Adel Al-Jubeir alisema Qatar haikuwa na nia ya kutekeleza matakwa hayo. "Tuko tayari kuzungumza na Qatar kuhusu utekelezaji wa matakwa, kuhusu utekelezaji wa kanuni, ikiwa Qatar ina nia, lakini imekuwa dhahiri kwamba haiko tayari," alisema waziri huyo katika mkutano na waandishi wa habari.

Mataifa hayo manne pia yameorodhesha kanuni sita wanzotaka Qatar itekeleze. Waziri wa mambo ya nje wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdurlrahman Al-Thani alipinga tamko la Jumapili kutoka kwa mataifa hayo na kusema vikwazo walivyoikwekea nchi yake vinakwenda kinyume na sheria za kimataifa.

Al-Thani alisema katika mahojiano na kituo cha Al Jazeera kwamba hakukuwa na dira ya wazi kutoka mkutano wa Manama, na kwamba kilichopo ni sera korofi kutoka mataifa yanayoizingira nchi yake na kukataa kwao kukiri kuwa hatua hizo ni haramu. Mapema Jumapili, gazeti la la al-Hayat lilisema likizinukuu duru zisizotajwa kutoka Ghuba, kwamba mataifa hayo manne yalitarajiwa kuweka vikwazo ambavyo taratibu vitaathiri uchumi wa Qatar.

Katar - Scheich Tamim bin Hamad Al Thani
Mfalme wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani wakati akitoa hotuba kwa njia ya Televisheni mjini Doha, Qatar, Julai 21,2017.Picha: Reuters/Qatar News Agency

Malumbano kuhusu Mahujjaji wa Qatar

Saudi Arabia imefunga mpaka wake wa nchi kavu na Qatar, huku mataifa yote manne yakikata mawasiliano ya angani na baharini na Doha, wakiitaka nchi hiyo inayosafirisha nishati ya gesi kwa wingi kuchukuwa hatua kadhaa kuonyesha inabadilisha sera zake.

Qatar imeituhumu Saudi Arabia kwa kuhatarisha safari ya hijja kwa raia wake kwa kukataa kuwahakikisha usalama wao. Julai 20 Saudi Arabia ilisema Waqatari wanaotaka kufanya hijja mwaka huu wataruhusiwa kuingia nchini humo, lakini ikaweka masharti fulani. Wizara ya Hajji ya Saudia ilisema Mahujjaji wa Qatar wanaowasili kwa ndege laazima watumie zinazokubaliana na Riyadh.

Pia watapaswa kuomba viza waakti wa kuwasili Jedda au Madina, ambavyo ndiyo vituo pekee kwao kuingilia katika taifa hilo la Kifalme. Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya masuala ya Kiislamu ya Qatar, raia 20,000 wa nchi hiyo wamejiandikisha kushiriki katika ibada ya hijja mwaka huu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri: Saumu Yusuf