1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yalaani mashambulizi ya Iran nchini Iraq

8 Januari 2020

Mataifa ya Magharibi yamelaani mashambulizi ya makombora ya Iran kwenye vituo vya kijeshi vya Marekani na majeshi mengine ya kigeni nchini Iraq, na kuyahimiza mataifa yanayohusika kuacha kuchochea mzozo.

https://p.dw.com/p/3Vu6d
US-Marin
Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS/US Marines

Kila kitu kiko sawa! Alisema Rais Donald Trump katika ujumbe wa Twitter mapema leo, na kuongeza kuwa tathmini ya maafa ya uharibifu ilikuwa inafanyika lakini akasisitiza kuwa hadi sasa mambo ni mazuri.

Katibu mkuu wa jumuiya ya kujihami NATO Jens Stoltenberg amelaani mashambulizi ya makombora ya Iran dhidi ya vikosi vya muungano, na kuitaka Iran kujizuwia na vurugu zaidi. Afisa wa NATO alisema hakuna kati ya wanajeshi wake nchini Iraq alieumizwa katika mashambulizi hayo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambaye amemuelezea Soleimani kama "gaidi mkuu wa Iran", amebainisha wazi kwamba Israel itajibu iwapo itashambuliwa. Iran ilitishia kuulenga mji wa Haifa, kaskazini mwa Israel iwapo Marekani itajibu mashambulizi ya leo.

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameliambia bunge kuwa Iran haipaswi kurudia mashambulizi hayo hatari na kipuuzi na kuongeza kuwa siyo juu ya Uingereza kuamua juu ya uhalali wa mashambulizi ya Marekani yaliomuuwa Soleimani kwa vile operesheni hiyo haikuwa ya kwao.

irakische Militärbasis Ain al-Assad
Kambi ya Ain al-Assad mojawapo ya maeneo mawili yaliolengwa na mashambulizi ya makombora ya Iran, Januari 08, 2020.Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Mohammed

"Shambulio hilo halikuwa la kutowajibika. Kwa miaka mingi, miongoni mwa mambo mengi, kuwapatia makombora waasi wa Kihouthi na kundi la Hezbollaj, ambayo wameyatumia kuwashambulia raia wasio na hatia, kuendeleza utawala wa  Assad nchini Syria na bila shaka kutoa vifa vya miripiko kwa magaidi, ambao waliwachinja wanajeshi wa Uingereza. Qassem Soleimani alikuwa na damu ya wanajeshi wa Uingereza kwenye mikono yake," alisema Johnson wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu.

Juhudi za kutuliza hali

Mapema, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Dominic Raab alionya kwamba vita nyingine Mashariki ya Kati italinufaisha tu kundi la Dola la Kiislamu na makundi mengine ya kigaidi. Mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alisema shambulio la leo ni mfano mwingine wa uchochezi na kuongezeka kwa makabiliano.

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya watakuwa na mkutano wa dharura siku ya Ijumaa kuhusu Iran, kujadili nini kanda hiyo inaweza kufanya kupunguza mzozo. Ofisi ya waziri mkuu wa Iraq ilisema ilipokea onyo rasmi kutoka Iran muda mfupi kabla ya mashambulizi ya leo, lakini taarifa hiyo imesema Iraq inapinga vitendo vyovyote vya ukiukaji wa mamlka yake na mashambulizi kwenye ardhi yake.

Kufuatia shambulio hilo la Iran, mashirika kadhaa ya ndege yameepuka kutumia anga za Iran na Iraq. Shirika la usimamizi wa usafiri wa ndege nnchini Marekeani, limesema limezipiga marufuku ndege zote zenye usajili wa Marekani kutoruka kwenye anga ya Iraq, Iran na eneo la Ghuba. Urusi pia imezishauri ndege kuepuka anga za iran, Iraq na ghuba za Uajemi na Oman.

Vyanzo: Mashirika