Uingereza, Ufaransa na Algeria waomba kikao cha dharura UN
16 Oktoba 2024Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy amesema kwenye taarifa kwamba Israel inalazimika kuhakikisha raia wanalindwa na njia zinakuwa wazi ili kuruhusu misaada ya kuokoa maisha kupitishwa na kuongezwa kuwa haya ni miongoni mwa masuala yatakayozungumzwa kwenye mkutano huo waliouitisha.
Amesisitiza kwamba hali ya kiutu ni mbaya mno kaskazini mwa Gaza na huduma muhimu nazo zinazozidi kupungua, wakati Umoja wa Mataifa ukiripoti kwamba chakula kilichoingizwa kwenye eneo hilo katika wiki mbili zilizopita ni kidogo mno.
Mjini Berlin, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wakimbizi wa Palestina, UNRWA Philippe Lazzarini amewaambia waandishi wa habari mjini humo kwamba shirika hilo limefikia ukiongoni, na pengine litasitisha shughuli zake katika Ukanda wa Gaza kutokana na hali kuzidi kuwa tete.
Anasema hajui ni lini hasa watashindwa kabisa, lakini wamekaribia mno. Lazzarini amesema UNRWA inakabiliwa na mchanganyiko wa mambo, kuanzia ukosefu wa fedha na vitisho vya kisiasa dhidi ya shughuli zake. Na zaidi ya hayo ni kitisho cha magonjwa na njaa kinachoongezeka kila uchwao.
"Njaa imetengenezwa na tunajua suluhu iwe ni kuruhusu misafara na vyakula iingie Ukanda wa Gaza ili kuepusha hali hiyo. Na sio chakula tu, ni mchanganyiko wa dhiki kutokana na vita, uharibifu, lakini pia mazingira machafu ambayo watu wanaishi, ambayo watu wanaweza kuambukizwa ugonjwa wowote." alisema Lazzarini.
UNRWA, inatoa elimu, huduma za afya na misaada kwa mamilioni ya Wapalestina walioko Gaza, Ukingo wa Magharibi, Jordan, Lebanon na Syria, lakini ina uhusiano tete na Israel, ambao umeharibika hata zaidi tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na Hamas.
Mjini Madrid, mataifa ya Umoja wa Ulaya yenye wanajeshi kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Lebanon, UNIFIL, yamesema ni "muhimu na ni suala la msingi" kutambua kwamba ni umoja huo pekee ndio wenye uwezo wa kuamua kuhitimisha muda wa ujumbe huo.
Soma pia: Israel yashambulia barabara kuu ya Syria -Lebanon
Waziri wa Ulinzi wa Uhispania Margarita Robles amesema leo kwenye mkutano kwa njia ya mtandao na wenzake 15 na kuongeza kuwa yeye pamoja na wenzake wanaunga mkono ujumbe huo, unaoongozwa na Italia na wenye maelfu ya wanajeshi kusini mwa Lebanon.
Hii ni baada ya ujumbe huo kushambuliwa na Israel hivi karibuni na kuutaka Umoja wa Mataifa kuwaondoa wanajeshi hao kwenye uwanja huo wa vita.