Mataifa yasaka amani Sudan Kusini
26 Desemba 2013Fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya kutolea huduma za matibabu, chakula, na pia kuongoza kambi za wakimbizi wa ndani, kwa mujibu wa Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kiutu ya Umoja wa Mataifa.
Vile vile zitatumika kwa ajili ya wakimbizi 200,000 wa Sudan ambao wamekimbia kwenye majimbo ya Unity na Upper Nile ya Sudan ya Kusini.
"Kuna kiasi cha wakimbizi wa ndani 90,000 waliotokana na mapigano ya siku kumi zilizopita. Hao ni pamoja na 58,000 waliojihifadhi kwenye majengo ya Umoja wa Mataifa," alisema Toby Lanzer, mratibu wa huduma za kiutu za Umoja wa Mataifa nchini Sudan ya Kusini.
"Hiki ni kipindi kigumu sana kwa watu wa taifa hili jipya, na ni muhimu sana kwa mashirika ya misaada kuwa na fedha yanayohitaji kuokoa maisha ya watu," aliongeza, akielezea matarajio yake kuwa wafadhili watachukua hatua za haraka kupata fedha hizo.
Maelfu wauawa
Umoja wa Mataifa unasema kwamba maelfu wameuawa nchini Sudan ya Kusini tangu tarehe 15 Disemba, pale ghasia zilipoanza baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar, kwa kujaribu kumpindua.
Machar alikanusha na kumshutumu Kiir kwa kuwaangamiza wapinzani wake. Vita vya madaraka vilichochea ghasia kati ya makabila mawili ya Nuer la Machar na Dinka la Kiir.
Siku ya Jumanne (tarehe 24 Disemba), Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha kuongezwa kwa walinda amani 6,000 kukabiliana na kitisho cha vita vya wenyewe kwa wenyewe, ingawa itachukua muda mrefu kwa fedha za kutuma wanajeshi hao kupatikana.
Juhudi za amani
Katika ujumbe wake wa Krismasi kwa njia ya vidio kwa watu wa Sudan ya Kusini, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, alisema nchi hiyo iko kwenye kitisho, ingawa haitasimama peke yake. Ban Ki-moon amesema Umoja huo utafanya kila uwezalo kuzuia ghasia kusambaa zaidi.
Tayari Umoja wa Ulaya umemteua mpatanishi maalum wa mzozo huo, Alex Rondos, ambaye anatarajiwa kuwasili Sudan ya Kusini baadaye leo (tarehe 26 Disemba).
Viongozi wa mataifa kadhaa ya mashariki mwa Afrika, wakiwemo wa Kenya na Ethiopia, wanatazamiwa kukutana katika mji mkuu wa Sudan ya Kusini, Juba, wakikusudia kuwakutanisha Kiir na Machar.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga