Matokeo rasmi ya Uchaguzi wa Zambia, kutangazwa leo.
2 Novemba 2008Bwana Banda anaongoza kwa asilimia 40 ya kura milioni 1.78 zilizohesabiwa dhidhi ya mpinzani wake Michael Sata mwenye asilimia 38.2 ya kura hizo zilizopigwa.
Matokeo hayo, yametangazwa na Tume ya Uchaguzi nchini humo kutoka katika majimbo 149 kati ya 150.
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini humo, Florence Mumba amesema matokeo rasmi yanatarajiwa kutolewa baadaye leo.
Kufuatia kuongoza katika kura hizo, Maafisa wa serikali nchini humo wamearifu kuwa Bwana Banda ataapishwa leo mjini Lusaka.
Kutokana na hali hiyo, Chama kikuu cha upinzani nchini Zambia kimeelezea nia yake ya kuiomba mahakama, kura za uchaguzi wa urais zihesabiwe upya, baada ya chama tawala kuongoza kwa kura chache.
Chama cha Patriotic Front cha, Michael Sata, kinadai kuwa uchaguzi wa Alhamis wiki hii ulikuwa na undanganyifu na kimewataka maafisa wa uchaguzi kusitisha kutangaza matokeo zaidi ya uchaguzi.
Malalamiko hayo ya upinzani yametolewa katika wakati ambao, Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC, imearifu kuwa uchaguzi huo, ulikuwa huru na wa haki.
Uchaguzi wa Rais nchini Zambia umefanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Levy Mwanawasa, kufariki dunia Agosti mwaka huu, kutokana na ugonjwa wa kiharusi.
Wakati huohuo, habari kutoka nchini humo zinasema, ghasia zimetokea katika mji mkuu wa Zambia Lusaka, usiku wa kuamkia leo, baada ya kutolewa kwa taarifa kuwa Kaimu Rais Rupia Banda anaaongoza kwa kura, badala ya kiongozi wa upinzani ambaye ndiye aliyekuwa akiongoza tabgu kufanyika kwa uchaguzi huo siku ya Alhamisi.