Matokeo ya awali Pakistan
19 Februari 2008Washirika wa Rais Pervez Musharraf nchini Pakistan yadhihirika hawatajipatia ushindi bungeni.Matokeo yasio rasmi ya uchaguzi wa jana wa Bunge yaliotangazwa katika TV kutoka wilaya 241 za uchaguzi ,chama cha Pakistan Muslim League-Quaid na washirika wake kinachompendelea rais Musharraf ,kimenyakua viti 57 tu.Isitoshe, hata kikinyakua viti vyote vilivyobakia kutangazwa hakitaweza kujipatia wingi katika Bunge lenye viti 272 na viti 70 vya wajumbe wa kuteuliwa.
Tayari mwenyekiti wa chama kinachoelemea upande wa rais Musharraf ameungama kushindwa.
“Wapigakura wamepitisha hukumu yao na tukikwa wademokrasia tumekubali hukumu yao.”-alisema Tariq Azeem, msemaji wa Pakistan Muslim League-Quaid –chama kinacheelemea upande wa rais Musharraf.
Matokeo haya ni pamoja na mwenyekiti wa chama Chaudhry Shujaat Hussain pamoja na takriban mawaziri wote wa zamani wa jamadari musharraf.Hata pia mshirika wake wa chanda na pete Sheikh Rashid hakuvuka salama na ufagio uliopitishwas jana na wapiga kura.
Kituo cha Tv kimetangaza kwamba chama cha marehemu Benazir Bhutto-Pakistan Peoples’ Party (PPP) kimenyakua viti 83 kile cha mpinzani wake Nawaz Sharif cha Muslim League-N viti 64 huku vyama vyengine vidogo vikishinda viti vilivyosalia.Kwahivyo, yaonesha chama cha Benazir Bhutto kimeibuka usoni kabisa kutoka uchaguzi wa jana.Swali linaloulizwa sasa ni iwapo upinzani utaweza mwishoe kujipatia thuluthi-mbili za kura Bungeni ili kumuangusha madarakani rais Musharraf.Swsali jengine ni iwapo vyama viku 2 vya Upinzani kile cha marehemu Bhutto na kile cha Nawaz Shariff cha Muslim League vitaunda serikali ya muungano.
Uchaguzi wa jana ulikua hatua ya mwisho ya dola hili la kinuklia kuelekea demokrasia chini ya utawala wa kiraia baada ya miaka 8 ya utawala wa kijeshi wa misukosuko ukiongozwa na jamadari asiependeza Pervez Musharraf.
Wafuasi wa upinzani walimiminika barabarani mapema hii leo wakipaza sauti za waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif na za Benazir Bhutto alieuwawa .Kwa jumla wapigakura wameonesha kutoridhishwa na utawala wa miaka 8 sasa wa jamadari Musharraf.Vipi jamadari hiyo ataitikia hukumu ya wapiga kura wa Pakistan –mshirika mkubwa wa Marekani katika vita dhidi ya ugaidi ni swali la kusubiri na kuona.Kwani, huenda siku zake nae zimemalizika.