1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini au uangalifu?

Maja Dreyer7 Juni 2006

Mzozo wa Iran, utawala wa Palestina na vita nchini Somalia – haya ndiyo masuala yanayozungumziwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

https://p.dw.com/p/CHVt

Katika mzozo juu ya mradi wa kinyuklia wa Iran, mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, jana aliwasilisha mapendekezo ya makubaliano kwa serikali ya Iran. Upande wa Iran umesema, mapendekezo hayo ni hatua nzuri lakini yenye maana nyingi. Juu ya hayo, gazeti la “Märkische Oderzeitung” lina maoni yafuatayo:
“Serikali ya Iran itapewa teknolojia ya kiwango cha juu ili kuendeleza uchumi wake mbaya na kutumia nishati ya kinyuklia kwa njia ya amani. Haya yote tu ikiwa itakubali kuacha kurutubisha madini ya Uranium, kwani silaha ya kinyuklia itaipatia Iran nguvu mno. Jibu la Iran itaonyesha kama kweli inajali kutengezea nishati au kama inataka kupata mamlaka ya kijeshi katika eneo la Ghuba.”

Mhariri wa gazeti la “Financial Times” ana mashaka akiandika:
“Tusidanganywe na majibu haya mazuri kutoka Iran yasiyo ya kawaida. Katika historia mara nyingi Iran ilionekana kukubali, lakini kwa kweli ililenga tu kuchelewesha majadiliano. Ikiwa safari hii Iran kweli inataka kutafuta suluhisho inaweza kutoa ushahidi rahisi sana, yaani kusimamisha kurutubisha madini ya Uranium mpaka mzozo utatuliwe.”

Gazeti la “Frankfurter Rundschau” lakini linasema:
“Matumaini yapo tena. Hivyo tunaweza kufupisha matokeo ya ziara ya Bw. Solana nchini Iran. Siyo tu kwamba Iran inaonyesha iko tayari kushiriki katika majadiliano, bali pia imesema ina matumaini mazuri kuwa mzozo huu utaweza kutatuliwa.”

Sasa tunaelekea Palestina ambapo rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas anataka kura ya maoni juu ya suala la kuitambua rasmi Israel ifanyikwe. Kuhusu mada hii, gazeti la “Reutlinger General-Anzeiger” limeandika:
“Chama tawala cha Hamas kinaweza kuvunjika ikiwa mzozo katika ya chama hicho kwa upande mmoja na chama cha ukombozi wa Palestina (PLO) pamoja na chama cha Fatah kwa upande mwingine utatokeo. Rais Abbas wa PLO anajua pia kwamba kura ya maoni inaweza kuharibu mamlaka ya serikali ya Hamas iliyochaguliwa katika uchaguzi wa kidemokrasia. Hivyo mgongano wa ndani utakuzwa zaidi.”

Na mwisho tunalinukuu gazeti la “Tageszeitung” la mjini Berlin ambalo linazungumzia vita nchini Somalia. Limeandika:
“Ni rahisi mno kusema kwamba ushindi wa wapiganaji wa Sharia mjini Mogadishu ni ushindi wa kundi la al-Qaida na hivyo ugaidi una mamlaka nchini Somalia. Wapiganaji wa kiislamu nchini humo hawataki kuendesha Djihad lakini hawa ni watu wanaotaka amani nchini Somalia na hawataki kuangalia tena nchi yao inavyoharibika zaidi. Hata hivyo, kutokana na ugawaji katika siasa ya ndani ulioimarishwa na Marekani sasa wanamapinduzi wa Kiislam watafurahia ushindi huo wa kundi la Sharia. Wapiganaji waliosaidiwa na idara ya ujasusi ya Marekani walishindwa – maana ya tokeo hilo lina umuhimu kupita mipaka ya Somalia.”