1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya kuwaokoa wavulana walionasa Thailand yadidimia

6 Julai 2018

Kundi la waokoaji wanaojaribu kuwaokoa wavulana wa timu ya kandanda ya vijana walionasa pamgoni Thailand wamekumbwa na msiba baada ya mpiga mbizi wa zamani wa aliyekuwa akisaidiana na kikosi cha uokozi kufariki dunia.

https://p.dw.com/p/30xz9
Thailand Rettungsaktionen der SEALS
Picha: picture-alliance/AP Photo/Tham Luang Rescue Operation Center

Sababu ya kufariki kwa mpiga mbizi huyo imeelezwa kuwa ni kukosa kwa hewa ya Oksijeni. Kifo chake kimeibua wasiwasi juu ya usalama kwenye operesheni ya kuwaondoa wavulana 12 na kocha wao wa timu ya mpira, kutoka kwenye pango hilo lililojaa maji kutokana na mafuriko.

Habari hizo za simanzi zimejiri wakati serikali ikijizatiti kuwaokoa wavulana hao huku ikiwa na wasiwasi mkubwa juu ya hali ya hewa inayozidi kuwa mbaya kutokana na kunyesha kwa mvua ya masika na kupungua kwa hewa ya Oksijeni mahali walikonasa vijana hao pamoja na kocha wao kwa wiki mbili sasa.

Maafisa wanasema uwezekano wa kuwaokoa vijana hao unazidi kuwa mdogo.

Thailand Rettungsaktionen der SEALS
Picha: Reuters/A. Perawongmetha

"Hatuwezi tena kungojea hali zote kuwa sawa kwa sababu hali hali ilivyo kwa sasa inatushinikiza kuchukua hatua," alisema kamanda wa jeshi la wanamaji kundi la wapiga mbizi Arpakorn Yookongkaew alipokuwa anazungumza na waandishi habari nchini Thailand.

Kamanda huyo amesema zamani walidhani kwamba wavilana hao wangeliweza kuendelea kukaa salama katika pango hilo kwa muda huku wakitafuta njia zaidi za kuwaokoa lakini kwa sasa hali imebadilika na hawana tena muda wa kupoteza.

Huku hayo yakiarifiwa madaktari wanaendelea kufuatilia kwa karibu hali vijana hao walio kati ya miaka 11 na 16 pamoja na kocha wao aliye na miaka 25.  Kundi hilo lilinasa pangoni baada yakuingia katika pango hilo kulizuru baada ya mechi ya kandanda tarehe 23 mwezi Juni.

Mvua ya masika iliokuwa ikinyesha ikatatiza juhudi zao za kujitoa katika pango hilo na kuzuwiya waokoaji kuwapata kwa takriban siku 10.  serikali ya Thailand kwa sasa inajitahidi kutoa maji yaliojaa pangoni humo huku maji yakiendelea kujaa na njia pekee ya kuwaokoa ni kupitia wapiga mbizi ambapo wataalamu wanasema ni hatari hata kwa wapiga mbizi walio na uzoefu.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP

Mhariri: Iddi Ssessanga