Matumaini ya Wazanzibari katika urais wa Samia Suluhu Hassan
19 Machi 2021Ni kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa mwanamke kushika wadhifa huo wa urais.
Baada ya kuapishwa kwa Mama Samia saa nne asubuhi, watu mbali mbali walifuatilia matangazo ya moja kwa moja yaliokuwa yakirushwa na vituo vya televisheni na kuonesha kufurahishwa kwao.
Baadhi ya watu walikuwa wakitoa kauli za kumshukuru Mungu kwa hatua hiyo iliyofikiwa huku wengi wakitoa maoni yao kuonesha matumaini makubwa na kumtakia kheri kwenye utumishi wake.
Watu ambao amefanya nao kazi wanamzungumzia Rais Samia kuwa ni mchapakazi, msikivu, mwenye tabia ya kuheshimu maamuzi yanayotokana na vikao na mtoaji maamuzi yasioumiza kutokana na kutumia busara zaidi kwenye uamuzi wake. Professa Mohammed Hafidh Khalfan ambayee ni mmoja wa waliofanya naye kazi, amesifia utendaji wake wa kazi.
Baadhi ya wanaharakati akiwemo Jamila Mahmoud ambaye ni mkurugenzi wa wanasheria wanawake (ZAFELA) wamefurahishwa na wanaona nafasi hiyo inaweza kubadilisha na kuleta mtazamo mpya wa kuondokana na mfumo dume.
Samia alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa makamu wa Rais na sasa ameongeza rekodi ya kuwa Rais wa kwanza Tanzania mwanamke.