Matumizi ya viwavijeshi kama chakula, yamepanda chati Zambia
18 Desemba 2013Viwavi jeshi ni wadudu wanaopendwa sana kwa chakula na watu wa Zambia, ambao wanakiri kuwa licha ya ladha yake kuwa nzuri, pia wana vitamini ya kutosha kiasi kwamba, moja ya matumizi yake wakisagwa, hutengenezewa uji wa watoto.
Bidhaa hiyo imepanda bei ghafla katika soko nchini humo, kutokana na kuhitajika kwake katika mataifa mengine ya kusini mwa Afrika, ambayo ni Afrika kusini, Zimbabwe, na Malawi na kufanya wachuuzi wa bidhaa hiyo kuingiza pato kubwa kutokana na mauzo wanayofanya.
Viwavi jeshi kuinua hali ya uchumi kwa wananchi
Viwavi jeshi nchini Zambia, ambavyo hupatika zaidi katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, kwenye miti ijulikanayo kama mopane, vinaitwa kwa jina la kienyeji la Ifishimu kwa Kibemba au Ifinkubala kwa Kichewa, vinauzwa kwa bei ya kuanzia kwacha 5 ya Zambia kwa kimoja, thamani iliyo chini ya dola moja, ambapo kwa ushuhuda wa mwanamama maarufu wa biashara hiyo mjini Lusaka, Dorothy Chisa anasema kwa siku anaweza kufanya mauzo yanayofika mpaka kwacha 600.
Umaarufu wa ulaji wa viwavijeshi, umefanya hata baadhi ya migahawa na hotel kubwa, kuweka katika orodha ya vyakula vinavyotumika na wateja, ili kuwavutia zaidi wazungu, kama ilivyo katika mojawapo ya hotel za kitalii kwenye maporomoka ya Victoria nchini Zambia, na mmoja wa migahawa iliyopo mjini Johanesburg, Afrika kusini.
Imefahamika kuwa wachuuzi mbalimbali wa viwavi jeshi hutoka mjini Lusaka, na kwenda eneo hilo la kaskazini mwa nchi hiyo, wanakopatikana kwa wingi wadudu hao, kwa ajili ya kuwanunua kwa jumla na kurudi mjini Lusaka na sehemu nyingine za nchi jirani ili kuwauza kwa bei ya juu zaidi.
Watoto kuacha masomo kwa kusaka viwavi
Aidha, kutokana na shughuli hizo za uuzaji wa wadudu hao kupamba moto nchini humo, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na gazeti moja nchini humo hivi karibuni, imefahamika kuwa mahudhurio ya watoto wa shule zilizopo kaskazini mwa nchi hiyo, yameshuka kwa asilimia 70, ambapo watoto hao huenda kusaka wadudu hao kwa ajili ya kuuza, na wengi wa wazazi wanawalazimisha watoto zao kuacha masomo kwa ajili ya shughuli hizo.
Kwa mujibu wa taarifa ya kitafiti iliyotolewa na shirika la chakula na kilimo Duniani FAO, imefahamika kuwa matumizi ya wadudu kama chakula kwa binadamu, yamesaidia kutoa lishe kwa watu wanaokadiriwa kuwa bilioni mbili Duniani. kiwango cha viinilishe vilivyopo katika viwavijeshi, huwa katika kila gramu 100, gramu 53 ni protini, gramu 15 mafuta na gramu 17 ni wanga
Ulaji wadudu kupunguza kasi ya uhaba wa chakula Duniani
Taarifa hiyo ya FAO inafafanua kuwa, zaidi ya aina 1900 za wadudu Duniani, wanapatikana katika nchi zenye hali ya hewa ya tropiki, na lishe zinazotokana na wadudu, zimesaidia sana kurutubisha afya za watu wengi wa maeneo ya hsali ya tropiki , kwani wadudu wengi wana kiasi kikubwa cha protini na ulaji huo wa wadudu umesaidia pia hata kutokuwa na matumizi makubwa ya ardhi kwa ajili ya uzalishaji wa chakula mbadala
Aina mbalimbali za viwavi jeshi zimekuwa zikitumika pia kama chakula katika mataifa ya Afrika Magharibi na Afrika ya kati.
Dr Francis Mupeta, ambaye ni katibu mkuu wa chama cha madaktari nchini Zambia, akiongea na shirika la habari la IPS, amesema, anashuhudia matumizi ya viwavi jeshi kama sehemu ya kitabibu kwa lishe bora na hata kama matumizi ya mlo wowote wa kiasili katika maisha yake ya kawaida, anaongeza kuwa mke wake ni mjamzito, na anapata hamu ya kula kutokana na kutumia sana viwavijeshi kama kitafunwa kinachompa hamu ya kula vizuri, na kutopata kichefuchefu, kiasi kwamba inabidi wanunue kiasi cha kumtosheleza kwa matumizi ya miezi mitatu.
Mwandishi: Diana Kago/IPS
Mhariri: Abdul Rahman