1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji mjini Homs

MjahidA1 Machi 2012

Koffi Annan asema atamuomba Bashar Al Assad kushiriki katika juhudi za jamii ya kimataifa kupata Suluhu nchini Syria. Wakati huo huo vikosi vya serikali vimeingia Baba Amr kuendeleza ghasia dhidi ya upinzani.

https://p.dw.com/p/14CL9
Machafuko Homs
Machafuko HomsPicha: AP/Local Coordination Committees in Syria

Kulingana na Upinzani nchini humo, vikosi hivyo vya serikali ya Bashar Al Assad vimeshambulia eneo la Baba Amr mjini Homs. Utawala wa Syria umeapa kumaliza wale wanaowaita Magaidi mjini humo. Mapigano makali kati ya majeshi yalio asi na yale yaliotiifu kwa serikali ya Assad yanaendelea katika eneo hilo.

Mji wa Homs watatu kwa ukubwa nchini Syria umekuwa ngome ya maandamano ya mageuzi tangu mwezi machi mwaka jana. Mamia ya wakaazi katika eneo hilo wameuwawa tangu kuanza kwa mashambulizi huko Februari 3 mwaka huu.

Awali Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya siasa, Lynn Pascoe, alitangaza idadi ya vifo Syria imefikia 7,500.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na mkuu wa zamani wa Umoja huo Kofi Annan
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na mkuu wa zamani wa Umoja huo Kofi AnnanPicha: dapd

Mauaji lazima yasimamishwe

Hata hivyo mjumbe mpya wa Umoja wa Mataifa na pia Jumuiya ya nchi za kiarabu Koffi Annan amesema mauaji lazima yasimamishwe nchini humo. Annan amesema anatarajia kukutana na Rais Bashar al Assad na atamuomba kushiriki katika juhudi za jamii ya kimataifa kupata Suluhu nchini Syria. Hata hivyo mjumbe huyo amesisitiza kwamba jamii ya kimataifa iliogawanyika iunge mkono mpango wake ili wapate suluhu ya kudumu juu ya Syria.

Annan amesema kitu cha muhimu kwa sasa ni kusitisha mapigano na kuhakikisha kuwa misaada ya kibinadamu inawafikia raia wa Syria.

Katibu mkuu huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan atakutana na mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu Nabil El Araby na kwenda katika miji mengine kabla ya safari yake ya mjini Damascus.

Mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu Nabil El Araby
Mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu Nabil El ArabyPicha: picture-alliance/dpa

Huku hayo yakiarifiwa mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi za Ghuba watakutana na mwenzao wa Urusi Sergei Lavrov, katika mji mkuu wa Saudia-Ryadh.

Mkutano huo utakaofanyika Marchi 7 utazungumzia maswala mbali mbali ya Syria ikiwa ni pamoja na masikitiko yao juu ya namna Urusi ilivyopinga azimio la baraza la Umoja wa Mataifa la kusitisha mapigano nchini Syria.

Mwandishi Amina Abubakar/ dpa/AFP

Mhariri:Hamidou Oumilkheir