Mauaji nchini Ujerumani: Idara za ujasusi zimefeli
23 Agosti 2013Watu 9 wenye asili ya kigeni waliuawa kwa kupigwa risasi nchini Ujerumani katika miaka ya mwishoni mwa 1990. Katika wakati huo mauaji hayo ya watu wenye asili ya Uturuki na Ugiriki yalidhaniwa kuwa yalifaywa na makundi ya uhalifu wa kupangiliwa.
Watuhumiwa kwa hiyo walikuwa hususan jamaa wa wahanga hao. Yalidhaniwa kuwa ni makundi ya mafia, magenge yanayojihusisha na biashara ya madawa ya kulevywa , na kuingiza fedha haramu katika mtandao wa kibenki, kwa hiyo uchunguzi wa idara za upelelezi ulielekezwa huko.
Watu watatu wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia waliokuwa wakitafutwa sana walijificha bila kuonekana katika miaka ya mwishoni mwa 1990.
Wafanya uhalifu
Katika wakati huo walikuwa wakitekeleza uhalifu wao kwa kuwauwa raia wa kigeni nchini Ujerumani. Idara za upelelezi hazikufikiria suala la hamasa za kibaguzi katika mauaji hayo, kama anavyoeleza Marcel Fürstenau katika maoni yanayosomwa na Sekione Kitojo.
Novemba 2011 polisi walipata miili ya watu hao watatu wa kundi hilo la imani kali za mrengo wa kulia wakiwa wamefariki. Wameamua kujiua ili kuzuwia kukamatwa kwao. Walikuwa wakiwakimbia polisi kwa kuwa walihisi kuwa wako karibu na kukamatwa.
Baada ya kundi hilo lililokuwa likiendesha mauaji likiwa linajiita National Socialist Underground, NSU kugundulika, hali ya fadhaa ilikuwa kubwa. Kwamba bunge la Ujerumani liliamua kuanzia mwaka 2012 kuunda kamati ya vyama vya siasa na bila kupata ushauri kutoka kwa idara za ujasusi , lilikuwa jambo la kutia moyo na la lazima.
Matokeo ya uchunguzi
Na matokeo ya uchunguzi huo yameonesha wazi hali ya kutisha. Idara za usalama nchini Ujerumani zimefanya uzembe wa hali ya juu na hivyo zimeshindwa katika wajibu wao. Hayo ndio maelezo ya tume hiyo ya bunge, na sababu za kushindwa huko kutimiza majukumu baada ya mwaka mmoja na nusu mzima wa uchunguzi wa kina na maelezo ya kiasi fulani.
Katika kuyachunguza mafaili kadha na jinsi ya uulizaji wa maswali , mara nyingi imeonekana kuwa kuna hali ya kupotosha, wanasema wanasiasa wanaounda kamati hiyo ya bunge. Ndio sababu kuna hali ya faraja kiasi kusikia kutoka kwa wabunge wa tume hii ya vyama wakitamka wazi kwamba kundi hili la wanazi mamboleo la NSU huenda lilikuwa likipata msaada kutoka kwa polisi ama kutoka idara za ujasusi.
Pamoja na hayo ni sahihi na muhimu kusikia kutoka kwa mkuu wa kundi hilo la uchunguzi la tume ya vyama kuwa mauaji yaliyofanywa na kundi hili la NSU ni kushindwa kusiko na mfano katika historia ya viongozi wa idara za upelelezi nchini Ujerumani.
Wakati bunge jipya litakapofanya kikao chao baada ya uchaguzi hapo Septemba 22 , ni matumaini kuwa wabunge wataliona suala la msimamo mkali wa mrengo wa kulia na ubaguzi ni masuala muhimu ya kuyapa kipaumbele.
Mwandishi : Marcel Fürtenau / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Josephat Charo