Mauaji ya Soulemani: Mataifa yatakaka utulivu na busara
3 Januari 2020Televisheni ya Taifa ya Iran imeripoti kuwa mbali na Jenerali Qassem Souleimani shambulio hilo limewaua watu wengine 10 akiwemo Jenerali mwingine, Kanali, Meja na Kapteni wa jeshi la Iran. Kauli za kutaka utulivu katika wakati huu zimetolewa baada ya kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei kuapa kuwa atalipiza kisasi.
Moja ya taasisi zilizotoa wito wa utulivu na kujizuia ni Umoja wa Ulaya ambapo rais wa Baraza la Umoja huo Charles Michel amezitaka pande mbili katika mgogoro huo kuepuka kuendeleza mvutano. Michel amesema hatari ya kuendelea kuchochea mvutano inaweza kusababisha ghasia zaidi katika eneo lote la Ghuba.
Nayo wizara ya ulinzi ya Ujerumani imesema wanajeshi wake wanaosaida kutoa mafunzo kwa vikosi nchini Iraq wametakiwa kutoondoka kwenye kambi zao baada ya kuuawa kwa kamanda wajuu wa Iran Qasem Soleiman.
Nao Umoja wa Falme za Kiarabu umetaka utulivu, busara na kuepuka hisia katika kushughulikia mgogoro huo . Umoja huo umetoa kauli yake kupitia waziri wa mambo ya ndani Anwar Gargash aliyeweka ujumbe huo katika ukurasa wake wa Tweeter. Ameongeza kuwa masuala yanayozikabili nchi za ukanda wa ghuba kwa kiasi fulani yanatokana na kutokujiamini.
Nchi nyingine zilizojitokeza kutoa wito wa utulivu baada ya shambulio dhidi ya Iran ni pamoja na Misri, huku Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akimsifu Rais wa Marekani Donald Trump kwa kutoa amri ya kumuua Jenerali Soleimani huko Baghdad.
Uturuki yaonya huenda mauaji ya Souleimani yakaongeza machafuko Ghuba
Kwa upande wake wizara ya mambo ya kigeni ya Uturuki imeonya kuwa mauaji ya Soleimani yaliyotokana na mashambulizi ya anga ya Marekani yataongeza machafuko ya kisiasa kwenye ukanda husika.
Wizara hiyo imeonya kuwa kuigeuza hasa Iraq kuwa eneo la mgogoro kutaathiri amani na usalama wa Iraq na ukanda wote.
Naye waziri wa mambo ya Kigeni wa Marekani, Mike Pompeo amesisitiza kuwa Marekani imemuua Kamanda huyo wa Iran ikiwa ni katika juhudi za kuzuia tishio la shambulio lililokuwa likipangwa na kamanda huyo. Pompeo amesema, Qasem Soleimani alikuwa akipanga vitendo ambavyo vingeweka maisha ya mamia ya Wamarekani katika ukanda huo hatarini. Hata hivyo hakusema ni lini ama wapi shambulio hilo lilipangwa kufanyika.