1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji ya mwandishi nchini Tanzania, doa au alama?

11 Septemba 2012

Tanzania iliaminika kuwa nchi isiyo sifa mbaya ya vurugu za kisiasa zilizoathiri jamii nyingi barani Afrika, bali mauaji ya mwandishi wa habari sasa yanaibua maswali ikiwa kweli dhana hii ilikuwa ya kweli au la!

https://p.dw.com/p/166rz
Jeshi la Polisi la Tanzania kwenye harakati za kupambana na waandamanaji.
Jeshi la Polisi la Tanzania kwenye harakati za kupambana na waandamanaji.Picha: AP

Mwisho wa juma hili Watanzania wamehitimisha shughuli ya sensa ya watu na makazi yao ambayo hapo mwanzo ilipangwa ichukue siku saba tu, kabla ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuongeza muda huo ili makarani wa sensa wakamilishe kazi yao.

Huenda kama muda huo wa sensa usingeongezwa, jumuiya ya wanahabari nchini wasingekuwa wakiomboleza wakati huu mauti ya kutisha na kushtusha yaliyomkuta mwenzao alipozingirwa na polisi.

Kifo cha Daudi Mwangosi ambacho kimetokea katika kijiji cha Nyololo, wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, tarehe 2 Septemba katika mazingira ambayo hayajaelezwa rasmi, kimeibua lawama nyingi kutoka sehemu na asasi mbalimbali za Tanzania. Sababu kubwa ni kwamba kimezidisha mlolongo wa matukio ya aina hiyo ambayo yanaweza kupunguza imani ya Watanzania katika mfumo mchanga wa demokrasia nchini.

Akiwa na umri wa miaka 42, Mwangosi tayari aliisha jenga jina lake kama ripota wa televisheni ambaye alikuwa na ustadi wa kuunganisha ujuzi na utambuzi wake kama mwandishi mwenye bidii ya kazi akijali usikivu na mtazamo wa wasikilizaji wa taarifa zake.

Siku hiyo ya msiba watazamaji wa Channel 10, kama sikosei, walitarajia taarifa yake kuhusu kampeni ijulikanayo kama M4C ya chama cha upinzani cha CHADEMA ambayo inalenga kuamasisha wafuasi wa chama.

Kampeni ilikuwa inaingia katika Mkoa wa Iringa lakini Jeshi la Polisi wakati huo huo lilizuia maandamano ya kisiasa kwa sababu ya sensa.

Lahaula ! Hicho ndicho kilikuwa kikomo cha maisha ya Mwangosi. Mkusanyiko wa CHADEMA uligeuza kijiji cha Nyololo kuwa mahali pa hatari na mara Mwangosi akaanguka ghafla, kulingana na taarifa ya aliyeshuhudia na akaona « tumbo lake limepasuka » kutokana na mlipuko.

Hakuna mwandishi wa habari Mtanzania aliwahi kabla ya hapo kuuliwa akiwa kazini. Mlipuko uliochukua uahi wa Mwangosi, kulingana na taarifa zilizotolewa mpaka sasa, ulitokea wakati mwanahabari huyo akiwa amizingirwa na kikundi cha polis ambao walikuwa wakiwasambaratisha wafuasi wa CHADEMA.

Nchi hii, inavyoelekea, imekuwa na orodha inayoongezeka ya matukio ya vurugu na vifo vya kisiasa, yakihusisha polisi na vyama vya upinzani. Matukio ya hivi karibuni yalikuwa Arusha, Singida, Songea na Morogoro.

Kila yanapotokea wanaharakati wa haki za binadamu na wanasiasa husema “jambo hili lisitokee tena” lakini mwelekeo wa vurugu hauishi, mbali ya kuongeza wasiwasi miongoni mwa raia ambao wanaona viongozi walio madarakani kama vile wanapuuza mambo yaliyofichika katika siasa.

Uchunguzi wa mazingira ya kifo cha Mwangosi hautakuwa umekamilika kama haukutoa mwelekeo wa jinsi ya kukomesha kurudiwa kwa vurugu za aina hii, hasa kuzuia utumiaji wa nguvu za polisi kupita kiasi lisiwe jambo la kawaida la siasa za Tanzania.

Uchunguzi huo usilenge kumtafuta mchawi ila kutoa mwanga katika maeneo yote ya kisiasa nchini, ikiwa pamoja na wale walio madarakani. Baada ya hapo kila upande ukabili ukweli kwa dhati, pakiwa na dhamira ya pande zote kuheshimiana na kudumisha uungwana.

"Matukio ya aina hii yanalitia aibu taifa letu," amesema Profesa Ibrahimu Lipumba, mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), wakati akieleza masikitiko ya chama chake kutokana na kifo cha Mwangosi. Akabainisha kuwa uongozi wa kisiasa wa Tanzania kwa wakati huu si wa kidemokrasia na hautendi haki kwa wote.

Kweli bila suluhisho la kisiasa na matumizi yasiyofaa ya polisi kubana sauti za upinzani na uhuru wa wananchi kukutana ni mambo yanayoweza kuzidisha vurugu ambazo zitakuwa ishara ya uongozi wa nchi kushindwa kazi.

Mapambano kati ya wafuasi wa vyama vya siasa na polisi yanaweza kufikiriwa kama mambo madogo lakini yana uwezekano wa kuashiria hali mbaya zaidi. Mwishowe, nani ataathirika kutokana na mwenendo huu – wahanga au wale watakaonusurika ?

Wakati umefika kwa raia wote wa nchi hii wajizatiti kukomesha mwenendo wa vurugu ambako wanaelekea kutumbukia. Wawe raia wa kawaida au serikali na majeshi yake wasiachiwe kutenda maovu bila aibu wala kuwajibishwa.

Hakuna shaka kuwa shauku ya haki za binadamu inazidi kuimarika katikia jamii ya Watanzania kwa sababu wanapenda amani na maendeleo. Wakati vyama vya siasa vinajiandaa kuwavutia wapiga kura kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015, Watanzania wanatamani kuthibitishiwa zaidi kwamba kweli mfumo wa demokrasia ya vyama vingi unafanya kazi.

Mwandishi: Anaclet Rweyagura/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef