1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawasiliano na serikali mpya ya Palestina

Mohamed Dahman24 Machi 2007

Utawala wa Rais George W. Bush wa Marekani uko makini kwa kiasi gani na uko tayari kuchukuwa hatua kwa kiasi gani kuwa na mawasiliano na serikali mpya ya umoja wa kitaifa ya Palestina?

https://p.dw.com/p/CB55
Waziri Mkuu Ismael Haniyeh akiwa na Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Palestina.
Waziri Mkuu Ismael Haniyeh akiwa na Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Palestina.Picha: AP

Hilo ni suala linaloulizwa na wachambuzi wa sera wa kigeni na wanadiplomasia na majibu yake bado hayako dhahiri wakati waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice akifanya ziara yake ya saba Mashariki ya Kati katika kipindi cha miezi minane iliopita.

Je utawala huo wa Bush umeazimia kuanza upya mchakato wa amani wa dhati kwa lengo la kufikia suluhisho la mwisho ambalo Israel na Wapalestina likiwemo kundi la Hamas watakuwa tayari kujifunga?

Au inapitia tu mapendekezo ili kuridhisha madai ya Saudi Arabia na washirika wengine wa Marekani wa madhehebu ya Sunni katika eneo la Mashariki ya Kati ya kuwepo mchakato wa amani unaonekana kufaa kama ni tuzo yao kwa kuunda ushirika dhidi ya ya kile afisa mmoja wa utawala huo wa Bush alichokielezea hivi karibuni kuwa kundi la pande nne la uovu la nchi za Iran, Syria na Hezbollah na Hamas yenyewe.

Daniel Levy mtaalamu wa Israel na mjumbe wa amani wa zamani anahisi kuna kitu kinachofanyika na kwamba anafikri Rice ana mamlaka kutoka kwa rais kuja na mpango lakini uwe wa kufaa na lazima ujumuishe mambo ya maana.

Kumekuwepo na harakati nyingi za kidiplomasia hususan huko Ramallah mji mkuu wa serikali ya Mamlaka ya Palestina licha ya pingamizi za Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert.

Olmert amekuwa akitaka kuendelezwa kwa susio la kidiplomasia la mwaka mmoja dhidi ya serikali yoyote inayoongozwa na Hamas hadi hapo serikali hiyo itakapokanusha hadharani matumizi ya nguvu, kulitambuwa taifa la kiyahudi na kuyakinisha kutimiza makubaliano ya amani yaliopita kati ya Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO na Israel.

Ikipuuza pingamizi hizo utawala wa Marekani hivi karibuni ulimtuma balozi wake mdogo alieko Jerusalem kwenda Ramallah kukutana na mojawapo ya maafisa waanadamizi wa serikali hiyo mpya ambaye ni Waziri wa Fedha Salam Fayyad.

Siku chache zilizopita Fayyad ambaye anataraji kushawishi mataifa ya magharibi sio tu kuanzisha tena uhusiano wa kibalozi na Mamlaka ya Palestina bali pia kuanza tena kutowa moja kwa moja msaada wa kiuchumi na wa kifedha pia ametembelewa na wajumbe maalum kwa Mashariki ya Kati kutoka Umoja wa Ulaya na balozi wa Umoja wa Mataifa kwa Norway.Norway sio nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya lakini ilianzisha mchakato wa amani wa Oslo mapema katika miaka ya 1990.Nchi hiyo ilidiriki hata kumtuma naibu waziri wa mambo ya nje kukutana na waziri Mkuu Ismael Haniyeh.

Wakati kundi la pande nne la amani ya Mashariki ya kati la Umoja wa Ulaya,Umoja wa Mataifa, Marekani na Urusi likisisitiza kwamba linatetea masharti matatu ya Olmert limesema kwamba serikali hiyo mpya ya Palestina itahukumiwa sio tu kwa muundo wake na sera bali pia kwa vitendo vyake ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za Rais Mahmoud Abbas kupigania kuwepo kwa mataifa mawili kama ufumbuzi wa mzozo wa Israel na Wapalestina.

Tokea Hamas iliposhinda uchaguzi wa bunge mwaka jana serikali ya Marekani imeungana na Israel kuongoza kuisusia serikali hiyo kidiplomasia na kwa misaada ili kudhoofisha madaraka na umashuhuri wake kwa kutaraji kwamba itanguka aidha katika uchaguzi mpya au kwa njia nyengine.

Lakini harakati hizo zimeshindwa kuzaa matunda na kama sio kuwa kukosa tija ambapo badala yake kundi hilo la wanamgambo wa Kiislam limezidi kuwa na nguvu kijeshi pamoja na kuungwa mkono na umma kiasi cha kuwa na uwezo wa kuhujumu mchakato wowote ule wa amani ambao inahisi kuwa hauzingatii maslahi yake vya kutosha.

Masuala yaliopo hivi sasa je serikali ya Marekani iko tayari kuliangalia upya kundi hilo na kuwa na msimamo usio wa uhasama? Je itaiwachia serikali hiyo mpya ya Palestina kujimarisha na kusonga mbele? Au upeo wa fikra wa kisiasa wa Rice ni kuun’gowa mkakati wa Hamas badala ya kuujumuisha?