Mawasiliano ya intaneti yadhibitiwa Congo
31 Desemba 2018Wakazi wa mji huo wamesema wanaamini kwamba serikali imechukua hatua ya kuzuia kuenea kwa habari. Mitandao pia imekuwa dhaifu huko mashariki mwa mji wa Goma. Mpaka sasa serikali haijasema lolote juu ya kadhia hiyo. Mnamo siku za nyuma serikali pia ilifunga shughuli za internet kwa madai ya kuzua uvumi, wakati ambapo maandamano yalikuwa yanafanyika.
Wapinzani nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo wamesema kwamba wanatumai mgombea wao atashinda kutokana na jinsi matokeo ya awali yanavyoonyesha.Hata hivyo mfungamano unaoongozwa na chama tawala umesema unao uhakika wa mgombea wao kushinda uchaguzi huo wa urais.Hali hiyo ya kutatanisha inatokana na vurumai iliyotokea hapo jana ambapo watu wengi hawakuweza kupiga kura kutokana na mripuko wa Ebola, ghasia na matatizo ya ugavi na usafirishaji.Uchaguzi wa safari hii ni wa kwanza kufanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, unaotoa fursa ya kuleta mabadiliko ya amani na
kidemokrasia nchini humo.
Meneja wa kampeni ya mgombea wa upinzani Felix Tshisekedi bwana Vital Kamerhe amedai kwamba Tshisekedi na mgombea mwengine wa upande wa upinzani Martin Fayulu wanaongoza, kila mmoja akiwa na asilimia zaidi ya 40 ya kura. Bwana Kamerhe amesema mgombea wa mfungamano wa serikali bwana Emmanuel Ramazan amepata asilimia 13 tu ya kura. Hata hivyo sehemu kubwa ya kura inasuburi kuhesabiwa.
Mkuu wa utumishi wa rais Kabila anayesaidia katika kampeni ya mjumbe wa serikali Ramazan Shadary, amewaambia waandishi wa habari wanao uhakika kuwa mgombea wao ameshinda lakini afisa huyo, hakutoa hesabu zozote.
Kambi ya upinzani ya bwana Fayulu bado haijatoa hesabu kamili lakini imeeleza kuwa mgombea wa serikali Shadary atakuwa anaota ndoto ikiwa anafikiri atashinda! Kulingana na utafiti wa maoni uliofanywa na kitengo cha Congo kwenye chuo kikuu cha New York, hadi ijumaa iliyopita Fayulu alikuwa anaongoza kwa asilimia 47 ya kura wakati Tshisekedi alikuwa na asilimia 24. Kulingana na utafiti huo mgombea wa serikali Shadary alikuwa na asilimia 19 ya kura. Tume ya taifa ya uchaguzi, CENI, imesema matokeo ya awali yanatarajiwa kutolewa hapo kesho.
Kwa jumla uchaguzi ulifanyika kwa utulivu licha ya kadhia za hapa na pale zilizosababisha vifo vya watu watatu mashariki mwa Kongo. Hata hivyo watu zaidi ya milioni moja na laki mbili hawakupiga kura kwenye ngome kuu tatu za wapinzani, ambapo tume ya uchaguzi imechelewesha upigaji kura kutokana na mripuko wa Ebola na ghasia lakini katika mji wa Beni ambao pia umekumbwa na maafa ya Ebola, watu walijipigia kura kivyao kuashiria upinzani dhidi ya uamuzi wa tume ya uchaguzi wa kuahirisha upigaji kura. Wananchi katika mji huo wamesema uamuzi wa tume ya uchaguzi hauna mashiko.
Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE/AFPE
Mhariri: Jacob Safari