Mawaziri wawili muhimu wajiuzulu Uingereza
6 Julai 2022Hii ni kufuatia kujiuzulu kwa mawaziri wawili muhimu waliosema hayuko imara kuiongoza serikali.
Waziri wa fedha Rishi Sunak na mwenzake wa afya Sajid Javid wamejiuzulu pamoja na mawaziri wengine wadogo wadogo wakisema hawawezi kuendelea kuwa serikalini kufuatia msururu wa sakata ambazo zimeukumba utawala wa Johnson katika miezi ya hivi karibuni.
Mawaziri hao wamejiuzulu dakika chache baada ya Waziri Mkuu Johnson kuomba radhi kwa kumteua Chris Pincher kama naibu kiongozi wa chama cha Kihafidhina bungeni. Pincher alijiuzulu kutoka kwenye wadhfa huo wiki iliyopita baada ya kutuhumiwa kuwapapasa papasa wanaume wawili akiwa amelewa.
Upinzani waongezeka dhidi ya Johnson katika chama cha Kihafidhina
Johnson anadaiwa kumteua Pincher kwenye wadhfa huo licha ya kufahamu fika madai yanayomkabili.
Idadi inayozidi kuongezeka ya wabunge katika chama tawala cha Kihafidhina wanasema, wakati umewadia wa Johnson kujiuzulu.
Ila Johnson ameonyesha azma yake ya kutaka kusalia uongozini kwa kumteua Nadhim Zahawi ambaye alikuwa waziri wa elimu, kama waziri mpya wa fedha, naye Steve Barclay aliyekuwa mkuu wa utumishi wa umma, ameteuliwa kuichukua nafasi ya waziri wa afya. Johnson pia tayari amezijaza nafasi zengine zilizokuwa zimeachwa wazi.
Upinzani anaopokea Johnson katika chama chake chenyewe utaonekana wazi baadae leo atakapofika mbele ya bunge kwa ajili ya kuulizwa maswali na baadae adadisiwe kwa masaa mawili na wenyekiti wa kamati za bunge.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Leba Keir Starmer ametaka nchi hiyo iingie kwenye uchaguzi ili kuchaguliwe viongozi wapya.
"Tunahitaji mwanzo mpya wa Uingereza, Tunahitaji mabadiliko ya serikali na serikali hii inasambaratika. Chama cha Kihafidhina ni chama fisadi na kumbadilisha mtu mmoja katika uongozi hakutaleta tofauti yoyote, hakutatatua matatizo yaliyopo. Wacha tuwe na mwanzo mpya, wacha tuwe na mabadiliko ya kweli ya serikali," alisema Starmer.
Asilimia 69 ya Waingereza wamtaka Johnson ajiuzulu kama waziri mkuu
Uongozi wa Johnson umekumbwa na sakata kadhaa katika miezi kadhaa iliyopita. Waziri mkuu huyo alitozwa faini na polisi kwa kuvunja sheria za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona. Mbali na hayo kulichapishwa ripoti iliyoichafulia jina serikali yake kutokana na tabia ya maafisa katika ofisi yake ya Downing Street waliovunja sheria za virusi vya corona kwa kuandaa sherehe za unywaji pombe.
Kura moja ya maoni ya taasisi ya Uingereza ya YouGov inaonyesha kwamba asilimia 69 ya Waingereza wanafikiri Johnson anastahili kujiuzulu kama waziri mkuu ila kwa sasa, baadhi mawaziri katika serikali yake wangali wanamuunga mkono.
Mwezi mmoja uliopita Johnson aliponea kura ya kutokuwa na imani nayeya wabunge wa chama chake na sheria za chama hicho cha Kihafidhina zinamaanisha kwamba hakuwezi kuitishwa tena kura hiyo dhidi yake hadi kipindi cha mwaka mmoja kitakapokwisha.
Chanzo: Reuters/AFP