Ujerumani yaregeza kamba
20 Februari 2015Waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani Wolfgang Schäuble aliwashangaza washirika wake wa Ulaya na mawaziri wenzake serikalini alipoitaja risala ya waziri mwenzake wa fedha wa Ugiriki kuwa ni mbinu za kudai misaada zaidi bila ya kukubali kufanya mageuzi na kufunga mkaja.
Lakini wakati mkutano muhimu wa mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro ukikurubia kuanza mjini Brussels ,kansela Angela Merkel,kupitia msemaji wake,amesawazisha mambo akimsifu wakati huo huo waziri wake wa fedha na kusema serikali yake ina msimamo mmoja.
"Risala ya waziri wa fedha wa Ugiriki inadhihirisha kwamba Ugiriki ingali bado inapendelea kupata msaada wa Umoja wa Ulaya" amesema msemaji wa kansela Merkel,bibi Christiane Wirtz na kuongeza tunanuku:"Risala hii ni dalili njema inayoturuhusu tuedelee kujadiliana."Mwisho wa kumnukuu.
Ameongeza kusema mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro wanaokutana jioni hii mjini Brussels wataendelea kujadiliana kwa msingi wa risala hiyo-akielezea wakati huo huo matumaini ya kuyaona mazungumzo hayo yakipelekea kufikiwa makubaliano pamoja na Ugiriki.
Alexis Tsipras ahimiza uamuzi wa kishitoria uchukuliwe
Kwa upande wake waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras ameliamia shirika la habari la Uengereza Reuters "ana hakika maombi ya serikali yake ya kurefushwa kwa miezi sita muda wa mpango wa misaada yatakubaliwa.Ametoa wito wa kupitishwa kile alichokiita "uamuzi wa kihistoria kwa mustakbal wa Ulaya" .
Alexis Tsipras amesema nchi yake imefanya kila liwezekanalo kufikia ufumbuzi kwa manufaa ya pande zote na kwa misingi ya kuheshimu mwongozo wa sheria za Umoja wa Ulaya na pia matokeo ya uchaguzi ya nchi wanachama.
Der Spiegel yaashiria uwezekano wa kujitoa Ugiriki na kanda ya Euro
Taarifa hiyo ya waziri mkuu wa Ugiriki imetolewa muda mfupi baada ya jarida la Ujerumani Der Spiegel kuripoti benki kuu ya Ulaya inajiandaa kukabiliana na uwezekano wa kujitoa Ugiriki na kanda ya Euro.Benki kuu ya Ulaya haijasema chochote kuhusu ripoti hiyo.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/dpa/
Mhariri: Mohammed Khelef