Mawaziri wa Fedha wa nchi za G7 wakutana jijini London
4 Juni 2021Mawaziri hao wa fedha wa nchi saba tajiri G7 wanaanza mkutano wa siku mbili mjini London kujadili njia za kufikia mkataba wa kimataifa juu ya kuongeza kodi kwa kampuni kubwa, ikiwa ni pamoja na kampuni za mitandao za Google, Facebook na Amazon.
Mkutano huo unaofanyika chini ya uenyekiti wa waziri wa fedha wa Uingereza Rishi Sunak unawakutanisha mawaziri hao ana kwa ana kwa mara ya kwanza tangu kuzuka janga la corona. Waziri wa fedha wa Uingereza Sunak amesisitiza umuhimu wa kukutana ana kwa ana na mawaziri wenzake kutoka Marekani, Japan, Ujerumani, Ufaransa, Italia na Canada kwenye mazungumzo hayo ya siku mbili.
Waziri Sunak ameelezea matumaini ya kupatikana makubaliano kwenye mkutano huo hasa kutokana na dhamira ya rais wa Marekani Joe Biden ya kutaka kampuni kubwa duniani zitozwe kodi zaidi. Hata hivyo changamoto kubwa ni namna ya kufikia makubaliano juu ya kuleta mageuzi katika mfumo wa kodi. Makubaliano hayo yatapaswa kuwasilishwa kwenye mkutano wa kundi la nchi za G20 utakaofanyika mwezi ujao nchini Italia.
Soma zaidi:Mataifa ya G7 yaungana kujadili vitisho vya ulimwengu
Marekani imependekeza kiwango cha chini kuwa ni asilimia 15 kwa kampuni 100 kubwa kabisa duniani. Waziri wa fedha wa Ufaransa Bruno Le Maire amesema inapasa kufikia makubaliano. Amesisitiza kwamba hiyo itakuwa hatua muhimu. Hata hivyo waziri wa fedha wa Japan Taro Aso amesema ana mashaka iwapo makubaliano yatapatikana kwenye mkutano huo wa mjini London.
Kwa upande wake Marekani inatarajia makubaliano kamili kupatikana kwenye mkutano utakaohudhuriwa na marais na mawaziri wakuu wa kundi la nchi wanachama wa G20 utakaofanyika nchini Uingereza kuanzia tarehe 11 hadi 13 mwezi huu.
Nchi zote zitanufaika ikiwa kampuni kubwa zinalipa kodi zaidi pale ambako zinafanya kazi na kuingiza fedha na siyo tu pale ziliposajiliwa au kwenye makao yake makuu. Marekani inataka kuondolewa kwa kodi ya huduma za kidijitali inayotozwa nchini Uingereza, Ufaransa na Italia. Marekani imelalamika kwamba sera hiyo inayalenga makampuni yake. Ikiwa makubaliano hayatafikiwa juu ya kodi hiyo ya kimataifa, bidhaa za anasa kutoka Uingereza, Italia na Uhispania zitakuwamo hatarini kutozwa ushuru wa asilimia 25 nchini Marekani baadae mwaka huu.
Soma zaidiMawaziri wa mambo ya kigeni wa G7 wakutana ana kwa ana
Ujerumani,Uingereza na Ufaransa ziko tayari kukubaliana na pendekezo la Marekani lakini zinataka kampuni kubwa kama ya Amazon nayo iingizwe katika mfumo huo wa kodi. Waziri wa fedha wa Ujerumani Olaf Scholz amesema kampuni zote, bila ya walakini zitapaswa kufuata sheria mpya.
Chanzo://RTRE