Mawaziri wa Nje wa ECOWAS wakutana kuijadili Senegal
8 Februari 2024Matangazo
Kikao hicho maalum cha Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) kinafuatia uamuzi wa ghafla wa Rais Macky Sall kuahirisha uchaguzi wa Senegal, wiki moja tu baada ya Burkina Faso, Mali na Niger kutangaza kuwa wanajiondoa katika jumuiya hiyo.
Baraza la Upatanishi na Usalama la ECOWAS limesema mawaziri watakutana katika mji mkuu wa Nigeria Abuja leo kujadili hali ya sasa ya usalama na masuala ya kiasasa katika kanda hiyo.
Haikufahamika jana kama waziri yeyote wa Senegal atahudhuria. ECOWAS imeihimiza Senegal - moja ya mataifa wanachama wake wenye utulivu - kurejea katika ratiba yake ya uchaguzi, lakini wakosoaji tayari wametilia shaka mwelekeo wa kundi hilo juu ya nchi wanachama wanaozidi kukaidi.