1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Mawaziri wa Nje wa G7 wakutana kuionya Urusi

11 Desemba 2021

Mawaziri wa mambo ya kigeni na maendeleo wa mataifa tajiri duniani (G7) wameapa kuichukulia hatua kali Urusi wanayoishutumu kuzidisha harakati za kijeshi katika mpaka wake na Ukraine. 

https://p.dw.com/p/447rS
Großbritanniens Außenministerin Liz Truss
Picha: Olivier Douliery/AFP

Katika mkutano huo ulioanza Jumamosi (11 Disemba) mjini Liverapool, mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Liz Truss, aliapa kwamba ulimwengu wa Magharibi na washirika wake "utachukuwa msimamo mkali dhidi ya wachokozi wanaosaka kuuhujumu uhuru".

"Mwishoni mwa wiki hii, mataifa ya makubwa kabisa ya kidemokrasia ulimwenguni yatachukuwa msimamo dhidi ya wachokozi ambao wanataka kuuhujumu uhuru na kutuma ujumbe wa wazi kwamba tuko pamoja," alisema Truss kabla ya mkutano huo wa kilele.

"Ninataka mataifa ya G7 kuongeza mashirikiano kwenye maeneo ya biashara, uwekezaji, teknolojia na usalama ili tuweze kuulinda na kuupeleka mbele uhuru na demokrasia duniani kote. Nitahimiza hilo katika siku chache zijazo." Alisema waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Uingereza.

Urusi kikaangoni

Russland Vladimir Putin
Rais Vladimir Putin wa Urusi.Picha: Mikhail Metzel/AFP/Getty Images

Mkutano huo wa siku mbili kaskazini magharibi mwa England ni mwa mwisho wa moja kwa moja wakati Uingereza ikiwa mwenyekiti wa G7 na unafanyika wakati dunia ikikumbwa na mitafaruku kadhaa.

Hatua ya Urusi kuongeza wanajeshi kwenye mpaka wake na Ukraine ndiyo ajenda kuu ya mkutano huo, sambamba na kukabiliana na vitisho vya China, kuzuwia mpango wa nyuklia wa Iran pamoja na  mzozo wa Myanmar ambako jeshi limechukuwa madaraka tangu Februari Mosi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken aliwasili tangu Ijumaa kwa ajili ya mazungumzo ya awali na mwenzake wa Uingereza, Liz Truss, na pia waziri mpya wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Annalena Baerbock.

Blinken kwenda ASEAN

Schweden | US Außenminister Antony Blinken
Antony Blinken, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani.Picha: Jonathan Nackstrand/AP Photo/picture alliance

Wiki ijayo, Blinken ataelekea kusini mashariki mwa Asia wiki ijayo kwenye ziara inayolenga kuonesha umuhimu ambao Washington inauweka kwenye mkakati wake wa kukabiliana na China.

Siku ya Jumapili (12 Disemba), mawaziri kutoka Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) watashiriki kwenye mkutano huo wa kilele wa G7 kwa mara ya kwanza katika kikao kitachohusika na masuala ya chanjo ya COVID-19, fedha na usawa wa kijinsia.

Korea, Australia, Afrika Kusini na India pia zitashiriki kama wageni maalum wa Uingereza kwenye mkutano huo wa G7, ambapo waalikwa wengi wakihudhuria kupitia mtandao kutokana na kuzuka kwa aina mpya ya kirusi cha corona cha Omicron.