1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Ulaya wajadili mapendekezo ya Brexit

Sekione Kitojo
20 Julai 2018

Mawaziri wa masuala ya Umoja wa Ulaya wamekutana kujadiliano kuhusu mapendekezo ya Uingereza juu ya uhusiano wa baadaye  baada ya nchi hiyo kujitoa kutoka Umoja huo, maarufu kama Brexit.

https://p.dw.com/p/31pqC
Belgien EU nimmt neuen Brexit-Plan aus London zurückhaltend auf | Michel Barnier
Picha: picture-alliance/AA/D. Aydemir

Mawaziri wa Umoja  wa  Ulaya  wanajiuliza  maswali kuhusiana  na  waraka  huo uliowasilishwa na serikali  ya  Uingereza.

Mawaziri  hao  wa  Umoja  wa  Ulaya  walijadili  leo mianya  iliyopo katika  majadiliano  ya  Brexit  na  Uingereza  wakati  mjumbe  wa Ujerumani  akikiri kwamba  ana  wasi  wasi  kwamba  muda unayoyoma  kabla ya kupata  makubaliano. Kiongozi wa  majadiliano ya  Brexit  wa  Umoja  wa  Ulaya  Michel Barnier alitarajiwa kuwafahamisha  mawaziri  hao  kuhusu  mazungumzo  aliyofanya  na mjumbe  mpya  wa  Uingereza  Dominic Raab, baada  ya  mkutano wao  wa  kwanza  jana Alhamis.

Belgien EU nimmt neuen Brexit-Plan aus London zurückhaltend auf | Blumel und Barnier
Kiongozi wa majadiliano ya Brexit wa Umoja wa Ulaya Michel Barnier(kushoto) akizungumza katika mkutano na waandishi habariPicha: picture-alliance/AA/D. Aydemir

Mapendekezo  ya  Uingereza  yanaangalia  kuhusu  eneo  la biashara  huru  la  pamoja  kwa  ajili  ya  chakula, ambalo litashuhudia  nchi  hiyo  ikikubali  viwango  vya  Umoja  wa  Ulaya, huku  ikikubali  taratibu  mbali  mbali kuhusu  huduma  ambazo zitaruhusu  Uingereza  kuweka  sheria  kwa  ajili  ya  sekta kama sekta  yake  kubwa  ya  masoko  ya  fedha.

Hata  hivyo , Umoja  wa  Ulaya  umekuwa  kila  wakati  ukisisitiza kwamba  Uingereza  haitaweza  kuchagua miongoni  mwa uhuru  wa kundi  hilo  la  mataifa: ikiwa  ni  pamoja  na  uhuru  wa  kusafirisha bidhaa, huduma, watu  na  mitaji.

Großbritannien Theresa May, Premierministerin
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May akizungmzia kuhusu Brexit bungeniPicha: picture alliance/dpa/Parliamentary Recording Unit/Parliamentary Recording

Makubaliano ya kujitoa EU

Mawaziri hawakutarajiwa  kuidhinisha  jibu lisilokuwa  rasmi  leo kuhusiana  na  waraka  huo  wa  Uingereza, ambapo  wanadiplomasia wa  Umoja  huo  waliyaeleza  mapendekezo  hayo  kuwa  ni  waraka mmoja  miongoni  mwa  mingi. Waziri  wa  Ufaransa  anayehusika  na masuala  ya  Umoja  wa  Ulaya  Nathalie Loiseau  akizungumzia kuhusu  mkutano  huo  alisema.

"Leo umuhimu wa  kwanza  ni  kufanyia  kazi  makubaliano  ya kujitoa. Tunapaswa  kuwa  tayari  mwezi  Oktoba  kuidhinisha makubaliano  ya  kujitoa kwasababu  baada  ya  hapo  yanapaswa kuidhinishwa nchini  Uingereza  na  tunapaswa  kuyaidhinisha  katika bunge  la  Ulaya. Kwa  hiyo  huo ndio umuhimu. Na natarajia  kusikia kile  ambacho  Michel Barnier atakachotuambia  juu  ya  kikao cha majadiliano."

Belgien - Brexit-Minister Raab und EU-Chefunterhändler Barnier
Waziri wa Brexit wa Uingereza Dominic Raab (kushoto) akizungumza akiwa na Michel Barnier wa Umoja wa UlayaPicha: Getty Images/AFP/J. Thys

EU imeweka mtazamo  wake  kuhusu  mahusiano  ya  baadaye mapema  mwaka  huu. Waziri  wa  masuala  ya  Umoja  wa  Ulaya wa  Ujerumani , Michael Roth , alisema  waraka  huo  unakwenda kinyume  na  miongozo ya  majadiliano  ya  Umoja  wa  Ulaya. Lakini miongozo hiyo sio msahafu,"  amewaambia  waandishi  habari  kabla ya  mazungumzo  hayo  leo. "Kuna  sheria, na  sheria  hizi zinapaswa  kufuatwa,"  waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa Luxembourg  Jean Asselborn  alisema. "Hatupaswi  kuzichezea. Kuna  mamia  kwa  maelfu  ya   ajira  hapa, au  zaidi. Na  kwa  hali hii  inahusu  uthabiti  barani  Ulaya,"  ameongeza.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe / dpae

Mhariri: Iddi Ssessanga