Mawaziri wa Umoja wa Afrika wakutana
21 Februari 2005Mbabane:
Mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje kutoka nchi 15 za Kiafrika leo wanaendelea na mkutano wao katika ufalme wa Swaziland wenye lengo la kutafuta mikakati ya kuafikiana kuhusu jukumu bora la Afrika kwenye Umoja wa Mataifa. Mkutano wa siku tatu unajadili mapendekezo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, ya kuleta mageuzi katika Umoja wa Mataifa na hasa kuongeza Wajumbe zaidi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Pendekezo mojawapo ni kuipatia Afrika viti viwili vya kudumu kwenye Baraza hilo. Afrika Kusini, Nigeria na Misri zimeonyesha ari ya kuiwakilisha Afrika ingawaje Mawaziri hao 15 wa Mambo ya Nchi za Nje hawatapendekeza majina ya wagombea. Wajumbe wa kamati walioteuliwa na Viongozi wa Umoja wa Afrika wakati wa mkutano mkuu uliofanywa Abuja mwezi uliopita ni kutoka Tanzania, Uganda, Angola, Botswana, Zimbabwe, Niger, Nigeria, Ghana, Senegal, Congo, Gabon, Kameroun, Rwanda, Libya na Algeria.