May aifafanulia Uingereza muafaka wa Brexit
27 Novemba 2018Waziri Mkuu Theresa May atazitembelea leo Ireland ya Kaskazini na Wales kama sehemu ya ziara ya Uingereza ya kutafuta uungwaji mkono wa muafaka wake wa Brexit unaokosolewa na wengi kabla ya kura ya bunge.
Ziara ya leo inajumuisha mikutano na viongozi wa kisiasa kutoka vyama vyote vya Ireland Kaskazini – ambayo ndiyo itayokuwa na mpaka pekee wa Uingereza na Umoja wa Ulaya na ambayo mustakabali wake umekuwa kizingiti katika mazungumzo hayo.
Katika taarifa ya kutangaza ziara hiyo na kutetea mipango ya mpaka iliyokubaliwa na Umoja wa Ulaya, May amesema baada ya kuambiwa na Umoja wa Ulaya kuwa Uingereza ingehitajika kugawanywa mara mbili, nchi hiyo inaondoka ikiwa moja.
Hapo jana waziri huyo mkuu alitoa ombi butu kwa wabunge wenye mashaka kuunga mkono mpango wake wa kuwachana na Umoja wa Ulaya, akisema kuwa sio mpango bora Zaidi, lakini ndio uliopatikana, na mbadala wake ni kutumbukia mahali pasipojulikana.
Aliliomba bunge kukubaliana nao na kusonga mbele, kwa ajili ya wapiga kura. May alithibitisha kuwa bunge litaupigia kura mswada huo Desemba 11,baada ya siku kadhaa za mjadala, kuhusu kama wayaidhinishe au wayapinge makubaliano hayo.
Utetezi wa May bungeni wa muafaka wake huo uliopatikana baada ya kazi ngumu ulifuatia mfululizo wa shutuma, kutoka kwa wanaungaji mkono sugu wa Brexit, wabunge wanaouunga mkono Umoja wa Ulaya na wabunge wasiokuwa serikalini wala upinzani ambao awali walikuwa watiifu.
Katika tukio jingine linaloweza kuwa pigo kwa May, Rais Donald Trump amesema makubaliano hayo yanaonekana kuwa muafaka mzuri kwa Umoja wa Ulaya, ambao utafanya iwe vigumu Zaidi kwa Uingereza kufikia makubaliano ya kibiashara na Marekani.
Katika kujibu kauli za Trump, ofisi ya May imesema chini ya mkataba uliofikiwa na Umoja wa Ulaya, Uingereza itakuwa na sera huru ya kibiashara ili nchi hiyo iweze kusaini mikataba ya kibiashara na nchi nyingine kote duniani – ikiwemo Marekani.
Lakini katika mjadala wa jana bungeni, wabunge kwa mara nyingine walielezea kutoridhika kwao, na mkataba huo unaioweka Uingereza nje ya Umoja wa Ulaya bila ya usemi wowote lakini bado ipo chini ya sheria na majukumu ya uwanachama hadi mwishoni mwa mwaka wa 2020 wakati mkataba mpya wa kudumu kuhusu mahusiano yao ukishugulikiwa.
Kiongozi wa chama cha Labour Jeremy Corbyn alisema muafaka huo mbaya utaiacha Uingereza katika hali mbaya Zaidi, bila kuwa na sauti kuhusu sheria za Umoja wa Ulaya na bila uhakika kuhusu mustakabali wake.
May alihoji kuwa watu wa Uingereza wamechoka na mijadala isiyokuwa na kikomo kuhusu Brexit, na kuunga mkono mktaba huo utawawezesha wananchi kuungana tena kama bila kujali ni upande gani walioupigia kura.
Wengi wa wabunge walionekana kutoshawishika. Wabunge kadhaa wa Conservative wanasema wataupinga mswada huo. Chama cha Democratic Unionist cha Ireland Kaskazini, ambacho ni mshirika wa serikali ya wachache ya May, pia kunaupinga kamatu vilivyo vyama vyote vikuu vya upinzani.
Uingereza na Umoja wa Ulaya zinasisitiza kuwa Uingereza haiwezi kuyajadili upya makubaliano hayo, na wapinzani wa mpango huo hawakubaliani kuhusu kinachopaswa kufanyika kama bunge litaupinga. Baadhi wanataka uchaguzi, wengine wanataka kura mpya ya maoni, na baadhi wanasema Uingereza iondoke Ulaya bila ya mkataba.
Mwandishi Bruce Amani
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman