1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

May apata wakati mgumu katika Brexit

Isaac Gamba
3 Septemba 2018

 Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Uingereza, Boris Johnson, ameendeleza mashambulizi yake hii leo  dhidi ya serikali ya Waziri Mkuu Theresa May akitabiri ushindi kwa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo kuhusu Brexit.

https://p.dw.com/p/34CkO
Kenia Treffen zwischen britischen Premierministerin Theresa May und dem Präsidenten Uhuru Kenyatta
Picha: DW/S. Wasilwa

Tangu alipojiuzulu wadhifa wake wa uwaziri wa mambo ya nje mwezi Julai, Boris Johnson amekuwa akiandika makala katika gazeti la Daily Telegraph akiikosoa serikali ya Waziri Mkuu May kuhusiana na mchakato wa mazungumzo kuhusu Brexit.

Johnson ambaye alikuwa mstari wa mbele wakati wa kampeni ya kura ya maoni kuhusu Brexit  na baadaye kushika wadhifa wa uwaziri wa mambo ya nje wakati Uingereza ilipoanza mazungumzo kuhusu Brexit amesema  anahofia kuwa matokeo ambayo hayaepukiki kuhusiana na mchakato wa Brexit  yatakuwa ni ushindi kwa Umoja wa Ulaya.

Wakati May akikabaliana na upinzani mkali ndani ya chama chake dhidi ya mpango wake wa kujiondoa katika soko la pamoja baada ya hatua ya Brexit lakini isalie katika biashara huru kwa baadhi ya bidhaa kupitia makubaliano yanayohusiana na ushuru wa forodha pamoja na taratibu nyingine kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya, hapo jana amesisitiza hatarudi nyuma kuhusiana na mpango huo na badala yake atapigania kupata muafaka na Umoja wa Ulaya.

May ameongeza kuwa atakubali kulazimishwa kukubaliana na masuala ambayo hayana masilahi kwa Uingereza.

Boris Johnson apinga mpango wa May

UK Boris Johnson
Boris Johnson waziri wazamani wa mambo ya nje wa Uingereza Picha: picture-alliance/empics/V. Jones

Hata hivyo, Jonson na kundi lake wanaupinga mpango huo wa May wakisema unaifanya Uingereza kuendelea kuwa karibu zaidi na Umoja wa Ulaya hata baada ya Uingereza kujiondoa kwenye umoja huo Machi mwakani.

Johnson ambaye kabla ya kujikita katika masuala ya siasa amewahi kuwa mwandishi wa habari akiliandikia gazeti la Daily Telegraph kwa miaka 20 amesisitiza kuwa mpango huo wa May ni janga la kitaifa mnamo wakati ukosoaji nchini Uingereza na katika Umoja wa Ulaya ukiongezeka kupinga mpango huo. 

Mazungumzo ya Uingereza na Umoja wa Ulaya kuhusu Brexit yamekwama hivi sasa katika masuala muhimu kadhaa ikiwa ni pamoja na jinsi gani pande zote mbili zitaweza kuzuia mazingira magumu yanayohusiana na mpaka kati ya Ireland ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya na Ireland ya Kaskazini na pia kuhusiana na hali ya baadaye ya mahusiano ya kibiashara kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Boris Johnson anasema suala linalohusiana na mpaka wa Ireland linatumiwa na pande zote mbili katika mazungumzo ya Brexit ili kuendelea kuibakiza Uingereza katika ushuru wa forodha na pia katika soko la pamoja. Johnson amesisitiza kuwa kashifa ni kuwa sio kwamba Uingereza imeshindwa katika mazungumzo hayo bali ni kuwa hata haijajaribu.

Hayo yote yanajiri mnamo wakati sarafu ya paundi ya Uingereza ikishuka thamani yake leo Jumatatu ikiwa ni baada ya kupanda thamani kwa kiwango cha juu ndani ya mwezi mmoja wiki iliyopita.

Mwandishi: Isaac Gamba /AFPE/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef