1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

May ataka ridhaa ya baraza la mawaziri kuhusu Brexit

14 Novemba 2018

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May anakutana na baraza lake la mawaziri kulishawishi juu ya mpango wake wa kukamilisha mchakato wa nchi hiyo kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya, lakini kunaonekana upinzani mkali.

https://p.dw.com/p/38FvT
UK Brexit | Ministerpräsidentin Theresa May im Unterhaus
Picha: picture-alliance/empics/PA Wire/V. Jones

Kansela Sebastian Kurz wa Austria, ambaye nchi inashikilia sasa urais wa Umoja wa Ulaya hadi mwishoni mwa mwaka huu, ameisifia rasimu ya mpango huo wa Theresa May, akisema kuwa mawaziri kutoka mataifa 27 ya Umoja huo wanaweza kukutana wiki ijayo kujadili hatua zinazofuata.

Akiyasifia makubaliano yaliyofikiwa hadi sasa kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza, Kurz amewaambia wanahabari mjini Vienna kwamba amezungumza na mkuu wa ujumbe wa Umoja huo kwenye mazungumzo ya Brexit, Michel Barinier, na maafisa wa Uingereza na kwamba anaamini kuwa kazi kubwa imeshafanyika.

Endapo kutakuwa na hatua yoyote miongoni mwa mabalozi wa Umoja wa Ulaya na Uingereza kwenyewe, mkutano wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya umepangwa kufanyika hapo Jumatatu. Kansela Kurz amesema viongozi wakuu wa mataifa wanachama wanaweza kukutana baada ya hapo.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Ireland, Leo Varadkar, Umoja wa Ulaya umepanga mkutano wa kilele tarehe 25 Novemba, ikiwa baraza la mawaziri litakubaliana na rasimu ya mpango wa Brexit unaowasilishwa leo na Waziri Mkuu Theresa May.

Wakosoaji wataka kura mpya ya maoni

Großbritannien Proteste in London | pro-Brexit
Waandamanaji wanaotaka Uingereza ijitowe moja kwa moja Umoja wa Ulaya haraka iwezekanavyo.Picha: Getty Images/AFP/T. Akmen

Wakosoaji wa May ndani ya chama chake cha Kihafidhina na nje wanapigania kura nyengine ya maoni kuwapa Waingereza fursa ya kuamua endapo kweli bado wanataka kuondoka Umoja wa Ulaya, ingawa leo akizungumza bungeni, May alirejelea msimamo wake wa kukataa kura nyengine ya maoni.

"Hatutapiga kura nyengine ya maoni. Hatutayatupa maamuzi ya Waingereza. Tutaondoka muungano wa forodha. Tutaondoka kutoka sera ya pamoja ya kilimo na tutachukuwa udhibiti wa pesa, sheria na mipaka yetu. Tutakamilisha mpango wa kuondoka na Uingereza inaondoka Umoja wa Ulaya tarehe 29 Machi 2019," alisema.

Hata hivyo, kuna wasiwasi endapo May ataweza kuwashawishi mawaziri wake kukubaliana naye, katika wakati ambapo upinzani dhidi yake ni mkubwa na wa wazi. Serikali yake ya wachache imemfanya kuwa kiongozi dhaifu kabisa kuwahi kushuhudiwa ndani ya kipindi kirefu katika siasa za Uingereza. 

Licha ya udhaifu huo, ana jukumu la kuhakikisha kuwa makubaliano ya kujiondoa Umoja wa Ulaya yanapitishwa baada ya miezi kadhaa ya majadiliano ndani ya Umoja huo. Pia yanapaswa kupitishwa na bunge kabla ya tarehe 29 Machi mwakani, ambao ndio muda wa mwisho uliowekwa na kanuni za Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman