1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na Haki

Uchaguzi wa Uingereza wagubikwa na mashambulizi ya kigaidi

Yusra Buwayhid
7 Juni 2017

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema jana kwamba yupo tayari kulegeza sheria zinazolinda haki za binaadamu, ili kurahisisha kuwasafirisha watu wanaoshukiwa kuwa ni magaidi.

https://p.dw.com/p/2eE7m
London Theresa May Erklärung Terroranschlag London Bridge
Picha: Reuters/K. Coombs

Theresa May ametumia moja ya hotuba zake za mwisho katika kampeni za kuelekea uchaguzi utakaofanyika Alhamis 8, kujadili  usalama wa taifa na kuonyesha msisitizo wake dhidi ya misismamo mikali ya dini ya Kiislam. May ameapa kuhakikisha kwamba vyombo vya usalama vinakuwa na nguvu wanayoihitaji kupambana na ugaidi.

Kauli hiyo ya May, imekuja siku chache baada ya shambulio kubwa la kigaidi likiwa ni la tatu kutokea nchini Uingereza mwaka huu. Watu saba waliuawawa baada ya washambuliaji kuendesha gari lao dhidi ya wapita njia na kuwagonga na baadae kuwachoma watu visu na kuwachinja baadhi yao kati kati mwa jiji la London.

"Ngoja kidogo niwaambie namaanisha nini. Namaanisha hukumu ya kifungo kirefu zaidi kwa kwa wale waliokutwa na hatia ya makosa ya ugaidi. Nakusudia kuzirahisishia kazi mamlaka husika kuwarejesha makwao matuhumiwa wa kigaidi. Na nakusudia  kuzuia uhuru wa kusafiri wa  watuhumiwa wa ugaidi ambao tutakuwa na ushahidi wa kutosha kwamba ni kitisho kwetu lakini hatuna ushahidi wa kutosha wa kuwafungulia mashataka mahakamani," amesema Theresa May

"Na kama sheria zetu kuhusu haki za binaadamu zinatuzuwia basi tutazibadilisha ili tuweze kufanya hivyo," ameongeza May.

Großbritannien Labour Chef Jeremy Corbyn
Kiongozi wa chama cha Labour Jeremy CorbynPicha: Getty Images/I. Forsyth

Mamlaka za Uingereza zilikabiliwa na raia wenye hasira Jumanne, baada ya polisi kutaja jina la mshambuliaji wa tatu wa shambulio la kigaidi la mwishoni mwa juma mjini London, ambaye Italia tayari ilishasema kwamba kuna uwezekano ni  mwanajihadi.

May anatabiriwa kushinda

Lakini hata kama waziri mkuu amekabiliwa na kampeni kali kuliko ilivyotarajiwa, chama cha Conservative bado kinaongoza katika kura za maoni ya raia.

Kwa mujibu wa kura zilizochapishwa Jumanne na kundi Survation, May ambaye wakati mmoja alikuwa anaongoza kwa alama 20 mbele ya chama cha Labour kwa sasa ameshuka kwa alama poja pkee - kutoka asilimia 41.6 hadi asilimia 40.4. Wakati huo huo, kundi lengine la Bookmakers limetabiri May atashinda kwa wingi mkubwa.

Katika kampeni zake, chama cha Conservatives kimemtangaza May kama kiongozi mwenye nguvu na mtu imara atakaye pambana mjini Brussels kwa niaba ya Uingereza baada ya taifa hilo kujiondoa katika Umaoja wa Ulaya na kuonya raia  kwamba Jeremy Corbyn kiongozi wa chama cha Labour  haiwezi kazi hiyo.

Hata hivyo umaarufu wa Corbyn  umeshika kasi wakati wa kampeni za uchaguzi na mara kwa mara amekua akivutia makundi kubwa ya watu katika mikutano yake.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/rtre

Mhariri: Bruce Amani