May awaandikia Waingereza waraka wa Brexit
25 Novemba 2018May, anayetarajia kufikia makubaliano ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya na kupata fursa ya mashirikiano ya baadaye na Umoja huo kwenye mkutano wa kilele wa Jumapili (Novemba 25) mjini Brussels, anakabiliwa na kitisho cha kukosa uungwaji mkono kwenye bunge la nchi yake.
Gazeti la Sunday Telegraph liliripoti kwamba wajumbe wa baraza lake la mawaziri na wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wanashirikiana kwa siri kuandaa mapendekezo ya "mpango mbadala", wakihofia kuwa wabunge wataukataa mpango wa sasa.
Lakini kwenye waraka wake huo uliochapishwa na magazeti kadhaa ya Uingereza, May alisisitiza kuwa makubaliano yake "yataheshimu matokeo" ya kura ya maoni ya 2016, ambapo asilimia 52 walipigia kura uamuzi wa kujiondoa na kwamba kitakuwa "kipindi cha kujijenga upya na maridhiano."
"Yatakuwa makubaliano yanayozingatia maslahi yetu ya taifa, ambayo yanaigusa nchi yote na watu wote, ama iwe ulipigia kura kuondoka au kubakia Umoja wa Ulaya," aliandika May.
"Ni makubaliano kwa ajili ya mustakabali mwema, yanayotuwezesha kuzitumilia fursa zilizo mbele yetu."
Akirejelea msimamo wake kwamba Uingereza inaondoka Umoja wa Ulaya ifikapo tarehe 29 Machi mwakani, waziri mkuu huyo aliwatolea wito Waingereza kuyaunga mkono makubaliano hayo.
"Bunge litakuwa na nafasi ya kufanya hivyo katika wiki chache zijazo pale litakapopiga kura muhimu juu ya makubaliano haya," aliandika May.
"Nitapigania kwa moyo na roho yangu yote kushinda kura hiyo na kuwafikishieni makubaliano ya kuondoka Umoja wa Ulaya, kwa maslahi ya Uingereza yetu na kwa watu wetu wote."
Upinzani mkubwa wa ndani na nje
Waziri Mkuu May anapania kukiunganisha chama chake tawala cha Conservative na washirika wao wa Democratic Unionist Party katika bunge la Ireland ya Kaskazini kwenye mpango huu.
Lakini wakati hayo yakijiri, vyama vya upinzani vya Labour, Liberal Democrats na Scottish Nationalists vimeapa kuyapigia kura ya hapana makubaliano hayo.
Kwa mujibu wa gazeti la Sunday Telegraph, mawaziri kadhaa wa ngazi za juu wanapanga kuwa na mahusiano ya mfano wa Norway na Umoja wa Ulaya.
Gazeti hili liliandika kuwa viongozi wa ngazi za juu wa Umoja huo wanapanga mkakati wa namna utakavyoongeza muda wa Kifungu Namba 50 - ambacho kinachotumika kuiondoa Uingereza mwezi Machi - ili kuruhusu uwezekano mwengine. Miongoni mwa hayo ni uwezekano wa kura nyengine ya maoni.
Akizungumzia waraka wa May, mbunge wa Labour Stephen Doughty alisema ni "uongo mtupu" kudai kuwa njia pekee iliyopo ni mpango wa May au kusiwe na makubaliano yoyote yale.
"Kwa kuyakataa makubaliano haya, bunge linaweza kuwapa wananchi chaguo la kweli kwenye uamuzi kuondoka Umoja wa Ulaya kwa masharti haya au kuendelea kubakia na makubaliano tuliyonayo ndani ya Umoja huo," aliongeza.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP
Mhariri: Caro Robi