May awataka wapiga kura kuunga mkono mpango wake wa Brexit
16 Novemba 2018Zaidi ya miaka miwili baada ya Uingereza kupiga kura kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya , bado haijafahamika ni vipi, katika masharti gani ama hata iwapo nchi hiyo itaweza kujitoa kutoka Umoja huo kama ilivyopangwa yaani Machi 29, mwaka 2019.
May ambaye aliingia katika wadhifa huo wa juu kutokana na mtafaruku uliofuatia kura ya maoni ya mwaka 2016, imeamua kufanya majadiliano kuhusu makubaliano ya Brexit ili kuhakikisha taifa hilo linajitoa kwa njia bora zaidi. Waziri wa fedha wa Ufaransa Bruno Le Maire amesema kila nchi ina haki ya kujitoa kutoka Umoja huo.
"Tunaweza kufanya, bila shaka. Kila nchi iko huru kuamua kujitoa kutoka katika soko hili la pamoja, kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya. Lakini kile Brexit inachoonesha ni kwamba gharama za kiuchumi za kujitoa katika soko la pamoja ni kubwa mno. Na kwamba kwa kweli wanadanganya na wanasiasa wasiowajibika nchini Uingereza ambao wanawaambia watu wa Uingereza kwamba Brexit itaishia katika hali bora ya hapo baadaye."
Sarafu ya Pauni yaporomoka
Nae waziri wa Brexit Dominic Raab alijiuzulu jana kuhusiana na makubaliano hayo, na kusababisha sarafu ya pouni kuporomoka. Wabunge waasi katika chama chake waliamua wazi kupinga uongozi wake na kumwambia wazi kwamba makubaliano ya Brexit hayatapita bungeni.
May, ambaye ameapa kubakia kuwa waziri mkuu, aliombwa na mwananchi mmoja aliyepiga simu katika redio LBC " kujiuzulu kwa heshima". Hakuweza mara moja kulijibu swali hilo la msikilizaji huyo. Waziri mkuu May aliwatolea wito moja kwa moja wapiga kura kuunga mkono mpango wake wa Brexit huku akipata changamoto kubwa kwa uongozi wake kutoka mahasimu wake katika chama chake.
"Kwa watu wengi waliopiga kura ya kujitoa," kile walichotaka kufanya ni kuhakikisha kwamba uamuzi kuhusu masuala kama nani anaingia katika nchi hiyo yatafanywa na sisi nchini Uingereza, na sio mjini Brussels, na hicho ndio hasa makubaliano niliyofikia yanachotoa," alisema May.
Waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte amesema leo kuwa Umoja wa Ulaya hautakuwa radhi kubadili makubaliano yanayopendekezwa ya Brexit iwapo yatatupiliwa mbali na bunge la Uingereza.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman