1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazingira mada tete mkutano wa G20

4 Julai 2017

Mazingira yanatarajiwa kupewa nafasi kubwa katika mkutano wa mataifa yenye nguvu ya kiuchumi G20 utakaofanyika Hamburg, Ujerumani. Ni baada ya Rais wa Marekani Trump kukataa makubaliano ya Paris.

https://p.dw.com/p/2fszJ
Hamburg - G20-Protestcamps
Picha: picture-alliance/dpa/C. Sabrowsky

Wiki hii, viongozi wa nchi 20 zilizo na nguvu zaidi kiuchumi na zinazoiunukia kiviwanda wanakutana mjini Hamburg, Ujerumani, miongoni mwao ni mwenyeji Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye amepewa jina Kansela wa mazingira na kwa upande mwingine Rais wa Marekani Donald Trump , kiongozi ambaye ameyataja mabadiliko ya hali ya hewa kuwa uongo mtupu na kuutamausha ulimwengu kwa kuiondoa Marekani kutoka makubaliano ya tabia nchi yaliyofikiwa Paris.

Ujerumani ikivalia joho la urais wa G20, Merkel haonekani kufumbia macho kile kinachoonekana kuwa suala tete. Serikali ya Ujerumani hivi karibuni ilitoa ajenda zitakazojadiliwa katika mkutano huo wa kilele wa G20, kwa kuthibitisha mabadiliko ya tabia nchi litakuwa mojawapo ya masuala makuu ya mazungumzo hayo. Alois Vedder mkuu wa idara ya siasa ya shirika la ulinzi wa wanyama pori duniani WWF ameiambia DW kuwa suala la tabia nchi litakuwa mojawapo ya ajenda kuu.

Suali ni je? Nini yatakuwa matokeo ya mkutano huo baada ya Marekani kujiondoa kutoka mkataba wa Paris? Ni vipi nchi nyingine 19 wanachama wa G20 zitasonga mbele bila ya Marekani? Je wataendelea kujitolea kutekeleza makubaliano hayo na kuhakikisha malengo yake yanafikiwa?

Macho yote kwa Trump

Waandamanaji nje ya Ikulu ya White House wakipinga uamuzi wa Donald Trump kuitoa Marekani kwenye mkataba wa tabianchi wa Paris
Waandamanaji nje ya Ikulu ya White House wakipinga uamuzi wa Donald Trump kuitoa Marekani kwenye mkataba wa tabianchi wa ParisPicha: Picture alliance/AP Images/S. Walsh

Mwaka 2020 una umihumu mkubwa kuhusiana na suala la tabia nchi. Ndiyo wakati ambapo Marekani inaweza kujiondoa rasmi kutoka mktaba wa Paris lakini pia ndiyo wakati ambao wanasayansi wanaonya kuwa utakuwa wa kuamua mustakabali wa mazingira duniani kwani iwapo viwango vya hewa chafu havitashuka, basi malengo yaliyofikiwa katika mktaba huo wa Paris ya kupunguza viwango vya joto duniani hadi chini ya nyuzi mbili havitaweza kufikiwa.

Wakati viongozi hao wenye ushawishi mkubwa duniani wakijiandaa kukutana Hamburg kwa mkutano wa siku mbili unaoanza Ijumaa na kukamilika Jumamosi, kuna shinikizo kubwa kutoka kwa umma, mashirika ya kijamii, wanasayansi na watu mashuhuri duniani kwa viongozi hao kuchukua hatua madhubuti za kuyalinda mazingira.

Misururu ya maandamano makubwa yanatarajiwa Hamburg wakati wa mkutano huo kuwashinikiza viongozi kuchukua hatua kupambana na umasikini duniani na kuyalinda mazingira lakini suali kubwa linasalia kuwa ni kwa kiasi gani hayo yatafikiwa bila ya Marekani mchafuzi wa pili duniani wa mazingira?

Wachambuzi watasubiri kuona iwapo hatua ya Trump kujiondoa kutoka mkataba wa Paris kutayumbisha kujitolea kwa nchi nyingine wanachama wa G20 au kutazipa nguvu kuhakikisha mkataba huo unafanikiwa katika malengo yake.

Biashara huru pia kujadiliwa

Kufikia sasa kumekuwa na ishara kubwa kutoka Umoja wa Ulaya na China kuwa ziko tayari kuonegza juhudi za kuyatakeleza makubaliano hayo na hata Marekani kwenyewe, miji na majimbo kadhaa yameahidi kupambana na ongezeko la joto duniani licha ya serikali kuu kutojishughulisha ipasavyo.

Nishati mbadala zinatakiwa kuchukua nafasi ya nishati zinazoharibu mazingir
Nishati mbadala zinatakiwa kuchukua nafasi ya nishati zinazoharibu mazingiraPicha: Picture alliance/ZB/P. Pleul

Aidha kurunzi pia itamulikwa kwa nchi kama Saudi Arabia na Urusi ambazo tangu jadi zimekuwa zikijikokota kuhusiana na suala hilo la tabia nchi. Saudi Arabia ni mshirika wa karibu wa Marekani na hivi punde imetia saini makubaliano ya kibiashara na utawala wa Trump wa kuuziwa silaha nan hivyo  ni muhimu kusubiri kuona ni kwa kiwango gani hayo yatashawishi mtizamo wake kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel amesema mkutano huo wa Hamburg utakuwa fursa muhimu ya kujua bayana kujitolea kwa nchi ikiwemo Marekani kuhusu biashara huru na mkataba wa Paris, akionya kuwa malubambano kuhusu masuala hayo mawili yataathiri kila mmoja ikiwemo Marekani.

Huku Ujerumani ikitafuta kuimarisha sura yake duniani kama mtetezi wa mazingira na mkombozi wa mktaba wa Paris ikijilinganisha na Rais wa Marekani asiyetabirika, suala la tabia nchi linatarajiwa kuibua hisia kali na kuibua matokeo yasitobirika katika mkutano huo wa G20.

Mwandishi: Ruby Russell

Tafsiri: Caro Robi

Mhariri: Iddi Ssessanga

 LINK: http://www.dw.com/a-39460270