Mazoezi makubwa ya kijeshi ya NATO yaanza Norway
25 Oktoba 2018Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo ya kujihami NATO Jens Stoltenberg amesema watafanya majaribio ya uwezekano wa kujibu changamoto za kiusalama, zinazosababishwa na Urusi tangu mwaka 2014, kufuatia nchi hiyo kuitwaa kimabavu rasi ya Crimea na pia hatua zake zinazoonekana kama jitihada za kuyumbisha usalama wa mataifa ya Magharibi.
Wanachana wote 29 wa NATO pamoja na nchi washirika Sweden na Finland watashiriki katika mazoezi hayo ya ardhini, majini angani na mitandaoni yanayoanza leo hadi tarehe 7 Novemba.
Kulingana na msemaji wa kijeshi wa Norway Ivar Moen tayari vikosi vyote vimekwishawasili na viko katika maeneo yao.
Zoezi hilo litawajumuisha wanajeshi 50,000, magari ya kijeshi 10,000 na zaidi ya ndege za kivita na meli 300 ili kulinda nchi wanachama kutokana na mashambulizi.
Nchi tano kubwa zinazochangia majeshi yake ni Marekani, Ujerumani, Norway, Uingereza na Sweden.
Urusi imekasirishwa na mazoezi ya kijeshi ya Jumuiya ya kujihami NATO
Urusi kwa upande wake imealikwa kutuma waangalizi nchini Norway, hatua ambayo Stoltenberg ameisifu akiitaja kuwa ya wazi.
Amesema iwapo Urusi itashiriki kwa heshima na kujiepusha na hatari yoyote haoni sababu ya taifa hilo kutoalikwa kufuatilia mazoezi hayo yanavyokwenda.
Hata hivyo Uruisi imekasirishwa na zoezi hilo huku Waziri wa wake wa ulinzi akionya kwamba huenda wakalazimika kujibu kufuatia shughuli zaidi zinazofanyika karibu na mpaka wake eneo la Magharibi.
Mapema mwaka huu Urusi iliandaa zoezi kubwa kabisa la kijeshi mashariki mwa nchi hiyo lililopewa jina la vostok.
Urusi inasema zaidi ya wanajeshi 300,000 walishiriki zoezi hilo lakini wanadiplomasia wa Magharibi wanasema idadi hiyo imeongezwa.
Mwandishi: Amina AbubakarIAFP/AP/dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga