Mazungumzo kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki Magazetini
26 Julai 2017Tunaanzia Brussels yalikofanyika mazungumzo kati ya wawakilishi wa Uturuki na wa Umoja wa Ulaya. Gazeti la "Rhein-Zeitung" la mjini Koblenz linamulika kilichotokana na mazungumzo hayo na kuandika: "Ufanisi mkubwa wa mkutano huo kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki ni ule ukweli kwamba umefanyika. Matokeo mtu asiyatarajie. Kwasababu hali imepotoka mno, viongozi wa mjini Ankara nao wamejitenganisha mno na mwongozo wa taifa linaloheshimu sheria. Umoja wa ulaya haujaregeza kamba na afadhali hivyo. Yeyote yule anaewakamata watu ovyo nchini mwake, anaetumia kesi mahakamani kuwa sehemu ya madaraka yake na yeyote yule ambae hataki kutambua misingi ya demokrasia ya mshirika wake, asitegemee ukarimu. Kwamba mazungumzo ya kujiunga Uturuki katika Umoja wa ulaya bado hayajavunjwa, sababu za hali hiyo si za kisiasa bali za kiutu. Hatua hiyo ingewaondoshea wananchi wa nchi hiyo ya Bosphorus, matumaini yote waliyokuwa nayo. Na wakati huo huo ingevuruga miradi ya maendeleo katika maeneo ambayo si ya wafuasi wa Erdogan."
Mzozo wa Harami Al Sharif haujamalizika
Mzozo uliochochewa na mitambo ya ukaguzi iliyowekwa na Israel katika eneo tukufu kwa waumini wa dini ya kiislam, kiyahudi na kikristo, la Harami Al Sharif mjini Jerusalem haujamalizika licha ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuamuru mitambo hiyo iondoshwe. Gazeti la "Badische Zeitung" linaandika: "Itakuwa shida kwa Netanyahu kuusifu mkakati wake kuwa umefanikiwa. Katika suala tete la nani ndie mwenye usemi katika eneo hilo la Harami al Sharif au Hekalu la Mlimani kama wayahudi wanavyoliita, amebidi kumeza machungu. Na suala hapo halihusiani pekee na mitambo ya ukaguzi bali zaidi kuliko yote ni suala la nani ndie mwenye haki miliki. Kimoja hata hivyo kinasalia pale pale, busara za kisiasa zingetumika tangu mwanzo basi pengine maisha ya watu wengi yangenusurika."
Ripoti kuhusu hisia za kizalendo
Mada yetu ya mwisho magazetini inamulika ripoti kuhusu hisia za wajerumani kuelekea siasa kali za kizalendo. Watu wameshusha pumzi, hisia hizo si kali hivyo ikilinganishwa na kwengineko barani Ulaya. Hata hivyo gazeti la "Schäbische Zeitung" linaandika: "Kwa maoni ya waratibu wa ripoti hiyo ya shirika la Bertelsmann, raia wa Ujerumani hawana haja ya kuingiwa na hofu ya vishindo vya wanaopinga demokrasia. Lakini mnamo mwaka wa uchaguzi mkuu, thuluthi moja ya wapiga kura wanaoweza kueneza hisia kama hizo , si idadi ndogo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo watu hao si wapinzani wa demokrasia bali wamevunjwa moyo na demokrasia. Na hilo pekee linatisha.Tukizingatia takwimu za ripoti hiyo inamaanisha kati ya watu milioni 61.5 wenye haki ya kupiga kura, kuna watu milioni 20 ambao baadhi yao hawana imani na umoja wa ulaya na mfumo wa demokrasia ."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga