1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo na Israel kikwazo kwa Umoja wa Wapalestina

23 Julai 2013

Wadadisi wanasema mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati yanayotarajiwa kuanza tena kutokana na upatanishi wa Marekani, huenda yakahujumu mchakato wa kuleta maridhiano baina ya Israel na Wapalestina.

https://p.dw.com/p/19DEG
Rais Mahmoud Abbas (kati kushoto)akizungumza na kiongozi wa Fatah Khaled Meshaal Cairo juu ya maridhiano Mei 2011.
Rais Mahmoud Abbas (kati kushoto)akizungumza na kiongozi wa Fatah Khaled Meshaal Cairo juu ya maridhiano Mei 2011.Picha: Picture-Alliance/dpa

Tangu yalipofikiwa makubaliano ya kuyaleta pamoja makundi ya kisiasa ya Hamas na Fatah 2011, bado juhudi za kuyaimarisha makubaliano hayo na kuundwa serikali ya Umoja wa kitaiaf hazijafanikiwa.

Mvutano wa hamas na Fatah

Chama cha Fatah cha Rais mahmoud Abbas chenye ngome yake ukingo wa magharibi na kile cha Kiislamu cha Hamas ambacho kinalidhibiti eneo la ukanda wa Gaza tokea 2007, vimekuwa katika mvutano na uhasama tangu 2007, lakini tokea kusainiwa makubaliano ya kuondowa hali hiyo yaliofikiwa nchini misri 2007, jitihada zimekuwa zikiendelea kujaribu kuunda serikali ya Umoja wa kitaifa.

Wapalestina wakiwa na vinyago vya sura za rais Mahmoud Abbas na Kiongozi wa Hamas Gaza, Ismail Haniya
Wapalestina wakiwa na vinyago vya sura za rais Mahmoud Abbas na Kiongozi wa Hamas Gaza, Ismail HaniyaPicha: AP

Kukubali kwa Rais Abbas kimsingi mnamo wiki iliopita kuanza tena mazungumzo ya amani na Israel baada ya miaka mitatu ya mkwamo,ni hatua iliyopokelewa kwa hasira na chama cha Hamas, ambacho ni adui mkubwa wa dola ya Israel. Chama hicho kimesema Abbas hana mamlaka ya kuzungumza kwa niaba ya Wapalestina wote.

Mitazamo

Mhadhiri wa siasa na historia katika chuo kikuu cha Kiislamu huko Gaza Walid al-Mudallal, amesema tukio hilo linaweza kulitanua zaidi pengo lilioko baina ya wapalestina na kuuvuruga mchakato wa maridhiano. Mnamo wiki iliopita, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry alitangaza kwamba Viongozi wa Palestina na Israel wamekubali kimsingi kuyafufua mazungumzo ya amani, kukitarajiwa kufanyika mkutano wa awali katika kipindi cha wiki moja , mjini Washington.

Hamas bila kupoteza muda kikatoa jibu, kikisema, hilo haliwakilishi takwa la umma wa Palestina na kwamba chama hicho hakitokubaliana na hilo.

Mhadhiri wa masuala ya siasa katika chuo kikuu cha Birzeit katika Ukingo wa magharibi samir Awad , amesema kurudi katika mazungumzo ya amani na Israel kutasababisha vikwazo vikubwa katika njia ya kuelekea maridhiano baina ya Wapalestina na kwamba hakuwa na uhakika kama kweli kutakuwepo na maridhiano.

Fikra za wenye shaka

Wenye shaka shaka na kufufuliwa mazungumzo ya amani, wanahisi jambo la busara kwanza ni kuleta maridhiano baina ya wapalestina ili kuwa na msimamo mmoja panapohusika na majadiliano na Israel. Wanadai mgawanyiko ndani ya Wapalestina ni jambo litakaloipa nafasi zaidi Israel kupoteza muda. Lakini kuna wanaosema kwamba mazungumzo na Israel sio jambo pekee linalokwamisha maridhiano baina ya Wapalestina. Wanasema utekelezaji wa mkataba uliosainiwa Misri ni mgumu kwa sababu ya matatizo ya ndani yanayoikumba Misri iliokuwa mpatanishi na hasa baada yamshirika wa Hamas Rais Mohammed Mursi kutoka chama cha udugu wa Kiislamu kuangushwa madarakani na wanajeshi.

Sherehe za mei 2011 katika mji wa Ramallah baada ya kufikiwa maridhiano kati ya Hamas na Fatah
Sherehe za mei 2011 katika mji wa Ramallah baada ya kufikiwa maridhiano kati ya Hamas na FatahPicha: picture alliance/dpa

Kwa mujibu wa mkataba kati ya pande hizo mbili, umekwama kutokana na mvutano juu ya kuundwa serikali ya mpito ya wataalamu wasiohusika na upande wowote, na hatimae kuandaliwa kwa uchaguzi wa bunge na rais katika muda wa miezi 12. sababu kubwa ni tafauti za maoni zilizozushwa na wanachama wa Hamas.

Wakosoaji wanasisitiza kwamba ukosefu wa maridhiano unatokana na kukosekana kwa utayarifu wa wadau wakubwa katika mgogoro huo baina ya fatah na Hamas.

Hamas kinakataa kumtambuwa waziri mkuu Rami hamdallah mwenye makao yake makuu mjini ramadhallah katika ukingo wa magharibi, badala yake kinamtambuwa kiongozi wake Ismail haniya kuwa waziri mkuu.

Chama hicho pia kilikuwa na msimamo kama huo hata wakati wa mtangulizi wa Hamdullah, waziri mkuu aliyejiuzulu Salam Fayyad. Suala hilo pia ni kikwazo kwa mazungumzo ya amani.

Aidha msimamo wa Hamas kuelekea Israel uko wazi. Haniya anayeiongoza serikali ya Gaza ameonya juu ya kile alichokiita, tahadhari ya kutoingia kwenye mtego mwengine wa Israel, akimtaka Rais Abbas awe na ujasiri wa kuunda mkakati wa Wapalestina , chini ya msingi wa serikali ya Umoja wa kitaifa.

Amesema kwanza ni lazima kumalizwe hali hiyo ya mgawanyiko kabla ya kuamua kuanza tena mazungumzo na Israel.

Marekani msimamizi wa mchakato huo wa mazungumzo baina ya Israel na Palestina, ina imani mazungumzo hayo yataleta matumaini . Waziri wa kigeni Kerry alisema ana matumaini kwa sababu Rais Abbas na Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wameonyesha nia ya kuanza tena mazungumzo.

Rais Obama akipeana mkono na rais Abbas na waziri mkuu Netanyahu-2009
Rais Obama akipeana mkono na rais Abbas na waziri mkuu Netanyahu-2009Picha: picture-alliance/AP

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa katika mashariki ya kati wanasema Kinachosubiriwa ni jinsi gani, hatua hiyo ya mazungumzo itaungwa mkono na wengi miongoni mwa wapalestina.

Waziri mkuu wa Israel ameashiria kwamba yatakuwa magumu, na kusisitiza kwamba makubaliano yoyote yatawasilishwa kwa umma wa nchi yake uamuwe katika kura ya maoni, lakini amesisitiza kwamba muhimu ni kuzingatia masilahi ya usalama wa dola ya Israel.

Mwandshi:Saumu Yusuf,afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman