Mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina kuanzishwa rasmi hii leo
28 Novemba 2007Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, amesema viongozi wa Israel na Palestina leo wataanzisha rasmi mazungumzo ya amani katika ikulu ya Marekani mjini Washington.
Kuanzishwa kwa mazungumzo hayo kunafanyika baada ya mkutano wa kihistoria kuhusu amani ya Mashariki ya Kati kufanyika mjini Annapolis katika jimbo la Maryland.
Katika mkutano huo viongozi wamekubaliana kwamba taifa huru la Palestina litaundwa kufikia mwishoni mwa mwaka ujao 2008.
Condoleezza Rice amesisitiza maneno yaliyosemwa na rais George W Bush kwamba maswala yote ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi yatatuliwa.
Rais Bush amesema huu ni wakati muafaka kuwadhihirishia Wapalestina kwamba ndoto yao ya kuwa na taifa huru inaweza kufikiwa katika meza ya amani. Aidha kiongozi huyo amesema kwa wakati huu machafuko yanayohubiriwa na wanamgambo wenye itikadi kali ni kikwazo kikubwa kinachozuia kuundwa kwa taifa huru la Palestina.
Rais Bush binafsi amesema amejitolea kwa dhati kutumia muda wake uliosalia kama rais wa Marekani kutafuta suluhisho la mataifa mawili la mgogoro wa Mashariki ya Kati.