John Kerry yupo mjini Paris
9 Mei 2016Mkutano wa kutafuta suluhu ya mzozo wa Syria baina ya Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault na mawaziri wenzake kutoka kundi la nchi zinazounga mkono Upinzani nchini Syria, unafanyika mjini Paris Ufaransa.
Jean-Marc Ayrault anakutana na mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia,Falme za Kiarabu na Uturuki katika jitihada za kufufua mazungumzo ya kuleta amani nchini Syria. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry anataraji kuwasili mjini Paris, japo haijafahamika iwapo atahudhuria mkutano huo. Taarifa kutoka ofisi ya waziri huyo zinasema kuwa kuna jitihada za kuandaa mkutano mwingine wa kimataifa utakaozikutanisha Urusi na Marekani pamoja na kundi la nchi zinazounga mkono upinzani. Msemaji wa ofisi yake Mark Toner amesema pamoja na kwamba Kerry atakuwa mjini Paris kukutana na Jean-Marc Ayrault, lakini hakuthibitisha ikiwa atahudhuria mkutano huo.
Makubaliano ya kusitisha mgomo gerezani
.Na taarifa kutoka kwa makundi ya haki za binadamu nchini Syria zinasema kwamba kumefikiwa makubaliano ya kusitisha mgomo katika gereza moja nchini humo, na wafungwa wapatao 800 ambao wengi wao ni wafungwa wa kisiasa. Chini ya makubaliano hayo wafungwa wasio na hatia wataachiwa huru
Wanasema mpango huo ambao umefikiwa siku ya jamapili utahitimisha uasi na mgomo uliofanywa na baadhi ya wafungwa katika gereza la Hama lililopo katikakati mwa Syria, ambao walikuwa wanapinga wafungwa wenzao watano kuhamishiwa katika gereza la Sadnaya kwa ajili ya kuhukumiwa kifo. Mmoja wa maafisa wa kundi la kutetea haki za binadamu ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema utawala umekubaliana na baadhi ya matakwa yao hasa ya kuwaachia baadhi ya wafungwa ambao hawana hatia.
Wafungwa 26 kuachiwa huru
Wafungwa hao waligoma wiki iliyopita na kuleta tafrani katika gereza hilo kabla ya hali kutulizwa kwa kurusha mabomu ya kutoa machozi. Kundi la uangalizi wa haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza limethibitisha kuwa chini ya makubaliano hayo wafungwa 26 wataachiwa huru.Hapo awali serikali iliwaachia wafungwa wenginie 46 katika makubaliano yaliyovunjika baadae. Hali katika magereza za nchi hiyo inatajwa kuwa mbaya ambapo umeme na maji hukatwa huku huduma za kimatibabu nazo zikiwa hafifu miongoni mwa wafungwa..
Wafungwa hao wanahofia iwapo wenzao watahamishwa katika magereza mengine watakumbwa na adhabu ya kifo. Makundi ya haki za binadamu yanasema wafungwa wengi wanashikiliwa katika magereza bila ya kuwa na hatia huku wengi wao wakiteswa, madai ambayo yanapigwa vikali na mamlaka
Kwingineko, waasi hapo siku ya jumapili wamerusha roketi katika eneo linaloshikiliwa na serikali mjini Allepo na kuwaua raia watatu na wengine 15 wakijeruhiwa. Mapigano hayo ni ya kwanza tangu kufikiwe makubaliano ya kusitisha mapigano hapo wiki iliyopita katika mji wa Allepo ambao umegawanyika majeshi ya serikali yakishikilia upande wa Magharibi na waasi upande wa Mashariki wa mji huo.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi
Mhariri:Iddi Ssessanga