Mazungumzo ya amani ya Afghanistan yawa ana kwa ana
15 Septemba 2020Pande hizo hasimu zinatafuta jinsi ya kufikia makubaliano ya kukomesha vita ambavyo vimedumu kwa takribani miaka 19 nchini Afghanistan.
Mazungumzo hayo yalifunguliwa rasmi Juma Mosi ambapo siku za awali kikundi kidogo cha wapatanishi kutoka pande zote mbili kilikutana kujadili kuhusu jinsi mazungumzo hayo yatakavyofanyika.
Hata hivyo mazungungumzo ya Jumamosi yalihusu tu uzinduzi wa majadiliano kati ya pande hizo mbili.
Majadiliano ya leo yanafanyika ana kwa ana kati ya wawawikilishi wa serikali ya Afghanistan pamoja na wale wa kundi la Taliban kuhusu jinsi ya kumaliza vita nchini Afghanistan na hatma ya nchi hiyo baada ya vita. Mkutano huo unafanyika bila ya kuwepo waandishi habari.
Masuala mbalimbali wanayoyajadili ni pamoja na masharti ya kuweka chini silaha, haki za wanawake na jamii za wachache pamoja na suala la kuwapokonya silaha maelefu ya wapiganaji wa kundi Taliban na wapiganaji watiifu kwa wababe wa kivita ambao baadhi yao wanaegemea upande wa serikali.
Mpatanishi mwandamizi wa upande wa serikali ya Afghanistan Nader Nadery amesema kikundi cha mawasiliano kinachojumlisha wajumbe kutoka kila upande kilifanya mazungumzo kuhusu sheria, muongozo pamoja na taratibu zitakazofuatwa katika mkutano wa leo.
Soma Zaidi:Huenda pande hasimu Afghanistan zikakutana Doha kwa mazungumzo
Naye msemaji wa kisiasa wa kundi la Taliban Muhammad Naeem ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kuwa mkutano wa leo utakuwa wa jumla na kwamba hakuna mambo makhsusi ambayo wameafikiana kujadiliana.
Hata hivyo afisa mmoja katika ofisi ya rais wa Afghanistan amesema mazungumzo ya leo yatalipa kipaumbele suala la kulishawishi kundi hilo kukubaliana kuhusu kukomesha vita nchini humo pamoja na kulitaka kundi hilo kupungunza vurugu. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo ambaye pia amehudhuria mazungumzo hayo amesema.
"Waziri Al Thani ninafuraha kubwa kukutana nawewe tena, tulikuwa pamoja wakati uliponikaribisha katika kufungua mazungumzo kati ya Taliban na Afghanistan. Ni hatua nzuri katika juhudi zetu Marekani na msaada wa Qatar kwamba mazungumzo haya sasa yameanza, na kwamba yataongozwa na kufanywa na Wafghanistan wenyewe.”
Hata hivyo, licha ya kuanza rasmi kwa mazungumzo hayo mwishoni mwa Juma, Afghanistan imeendelea kushudia vurugu na ghasia.
Majadiliano kati ya Taliban na uongozi wa kiasiasa mjini Kabul, yalipaswa kuanza muda mfupi baada ya makubaliano ya mnamo Februari baina ya Marekani na kundi hilo lakini yalicheleweshwa kwa miezi kadha kutokana na Taliban kuendelea kufanya mashambulizi pamoja kutoelewana kati ya serikali na Taliban kuhusu kuachiliwa kwa wafungwa wa kundi hilo.
Wakati huo huo, rais Donald Trump wa Marekani, katika kampeni zake za kutaka achaguliwe tena ameahidi kukomesha vita vya nchini Afghanistan na pia kufahamisha kuwa nchi hiyo itawaondoa wanajeshi wake wote walioko Afghanistn ifikapo Mei mwakani, kwa masharti kwamba kundi hilo litaheshimu na kuacha kufanya mashambulizi.
Mashirika: Reuters/AP