Mazungumzo ya amani ya Syria yafunguliwa Geneva
23 Februari 2017Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Staffan de Mistura alifanya mikutano tofauti na wawakilishi wa ujumbe wa serikali na upinzani leo asubuhi katika ofisi za Umoja wa Mataifa nchini Uswisi. Siku moja kabla, Mwanadiplomasia huyo alipuuza matumaini ya kupatikana makubaliano ya moja kwa moja katika mazungumzo hayo, lakini pande zote zinafahamu kuwa mienendo nchini Syria imebadilika tangu mazungumzo yaliandaliwa mara ya mwisho Geneva mwezi Aprili.
De Mistura anataka pande zote kujadili uwezekano wa kuundwa serikali ya pamoja ya mpito, katiba mpya na kuandaliwa uchaguzi. Duru za upinzani zimesema mikutano ya kwanza leo ilihusu ufafanuzi wa ajenda halisi ya mazungumzo hayo. Mmoja wa wajumbe wa upinzani Abdulahad Astepho amesema waasi watakuwa na jukumu kubwa katika duru hii ya mazungumzo.
Mazungumzo ya Geneva yanakuja baada ya mashauriano ya Astana, mji mkuu wa Kazakhstan, ambayo yaliratibiwa kwa kiasi kikubwa na Uturuki, mshirika wa karibu wa upinzani katika vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe, na Urusi, ambayo mashambulizi yake ya angani yanawasaidia wanajeshi wa sewrikali ya Rais Bashar al-Assad. Ni duru ya nne ya mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa tangu mapema mwaka jana.
Wakati hayo yakijiri, wanaharakati wameripoti leo kutokea mashambulizi makali katika mji wa kusini wa Daraa baina ya wanajeshi wanaoiunga mkono serikali na makundi ya upinzani yanayoongozwa na kundi la al-Qaeda. Mashirika ya habari ya upinzani pia yameripoti mashambulizi ya anga yaliyofanywa na serikali karibu na eneo la Hama, katikati ya Syria.
Serikali inasisitiza kuwa mpango wa kusitisha mapigano hauyalindi makundi yenye mafungamano na mtandao wa al-Qaeda, wakati waasi wanasema makubaliano waliyosaini mjini Ankara yanayahusisha makundi hayo.
Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia Watoto – UNICEF limetoa wito kwa pande zote katika mgogoro wa Syria kuwalinda watoto katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita. Karibu watoto milioni 10 wa Kisyria wanaoteseka moja kwa moja na madhara ya kila siku ya mgogoro huu mkubwa wanataka kitu kimoja tu: amani irejee na wafurahie tena maisha yao ya utotoni.
Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Gakuba Daniel